NA ASYA HASSAN

MKUU wa Mkoa Kusini Unguja, Rashid Hadidi Rashid, amewataka Walimu Wakuu wa skuli za msingi na sekondari za wilaya ya Kati kusimamia uwajibikaji wa walimu na kuhakikisha wanakamilisha mitaala kwa wakati.

Ameeleza kuwa kufanya hivyo kutapelekea walimu hao kukamilisha ufundishaji na vipindi wanavyopangiwa kwa wakati.

Akizungumza katika kikao cha pamoja cha kutathmini matokeo ya mitihani kwa mwaka 2020 katika ukumbi wa chuo cha walimu (TC) Dunga, kilichowashirikisha Walimu Wakuu na wasaidizi wao wa ngazi ya maandalizi, msingi, sekondari pamoja na viongozi, watendaji na maafisa wa mkoa huo.

Hadid alieleza kuwa hakuridhishwa na matokeo ya kidato cha nne ya mwaka uliopita kutokana na wanafunzi wengi mkoani humo kufanya vibaya.

Alifahamisha kwamba kutokana na hali hiyo ipo haja ya kushirikiana kati ya walimu, wazazi na wadau ili waweze kuandaa mikakati madhubuti itakayosaidia kupunguza tatizo hilo.

Sambamba na hayo, Hadid alifahamisha kwamba licha ya kuwepo kwa baadhi ya changamoto inayoikabili sekta ya elimu, wapo baadhi ya walimu wanashindwa kuwajibika ipasavyo na kutokamilisha vipindi vyao hasa kwa walimu wa skuli za msingi.

“Hali hiyo inapelekea kujitokeza kwa tatizo la baadhi ya wanafunzi kutojua kusoma, kuhesabu na kuandika wanapofikia elimu ya sekondari na kusababisha kutofanya vizuri katika mitihani yao ya taifa,” alisema.

Akizungumzia tatizo la udhalilishaji wa watoto katika maeneo ya skuli ambalo limekuwa likiendelea kushamiri siku hadi siku kwa baadhi ya skuli za wilaya hiyo, aliwataka walimu kuwa karibu na kufuatilia nyenendo za watoto hao ili kuwanusuru na suala hilo.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kati Unguja, Marina Joel Thomas na Katibu Tawala wa mkoa huo, Fatma Mohammed Juma, walisema ni vyema Walimu Wakuu wakaacha muhali na kuwachukulia hatua za kinidhamu walimu ambao watashindwa kutekeleza vyema majukumu yao.

“Kuoneana muhali na kutochukuliana hatua ndiko yanayosababisha kupatikana kwa matokeo hayo, hivyo ni vyema kuhakikisha kila mtu anawekewa mikakati ili aweze kuwajibika katika nafasi yake,” alisema Marina.