NA TATU MAKAME

SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar imeombwa kuingilia kati mzozo wa waliokuwa watumishi wanne katika Chuo cha Mafunzo ili waweze kupata haki zao.

Wafanyakazi hao wanadai walitakiwa kuacha kazi kisha kuandikiwa barua ya kustahafu na kulazimishwa kusaini bila ya ridhaa zao, hali iliyosababisha kukosa haki zao.

Akizungumza na gazeti hili, mmoja kati ya wafanyakazi hao aliyejitambulisha kwa jina la Shaali Khamis Saidi alisema kitendo cha kulazimishwa kuacha kazi kimewanyima uwezekano wa kupata haki zao.

Alisema aliajiriwa mwaka 2003 katika kikosi hicho cha Mafunzo akiwa mwalimu wa vijana wanaoingia kazini na ilipofika mwaka 2011 alilazimishwa kusaini barua ya kuacha kazi.

Alisema ilipofika mwaka huo 2011 alipangiwa kazi kwenda Kisiwani Pemba baadae alipatwa na dharura za kuuguliwa na mzazi wake na kuomba ruhusa kurudi Unguja ndipo mmoja kati ya wakuu wa kikosi hicho kumlazimisha kuacha kazi kwa madai ya kuwa hataki kufanya kazi.

Shaali aliwataja watu wengine walioachishwa kazi kuwa ni Ramtula Mossi Makame, Mbaraka Makunga Ndekeja na Mussa Haji Mohamed ambao kati ya hao wawili waliandikishwa katika mafaili ya wafanyakazi waliofariki.

Alisema kitendo hicho kimewasikitisha kutokana na kuwa umri wao bado unawaruhusu kuwepo kazini hadi sasa na wawili kusingiziwa kuwa wamefariki hali ya kuwa wako hai.

Hata hivyo alibainisha kwamba walifuatilia haki zao za kiinua mgongo baada ya mmoja kati ya wakuu wa kikosi hicho kumueleza kwamba fedha za kiinua mgongo aliingiziwa benki ya watu wa Zanzibar (PBZ) bila ya kupata fedha hizo hali iliyowapa manung’uniko makubwa.

Hata hivyo alisema mbali ya kufuatilia haki yake hiyo yeye na wenzake walishindwa kupata haki zao licha ya kufika mahakama kuu Zanzibar Vuga kufuatilia.

Hata hivyo Shaali aliiomba serikali kuingilia kati kufuatilia kiinua mgongo chao pamoja na pencheni kwani sheria ya mtumishi wa serikali baada ya mfanyakazi kustahafu hupatiwa pencheni lakini wao hawapati.

Katibu Mkuu wa shirikisho la Wafanyakazi (ZATUC) Khamis Mwinyi Mohamed alisema mtu yoyote ambae alifanya kazi serikalini ana haki ya kupatiwa haki zake.

Hata hivyo aliwataka wakuu wa vikosi vya serikali ya Mapinduzi Zanzibar na wale ambao wanasimamia haki za wafanyakazi kuhakikisha wanafanya haki katika kuwapatia stahiki zao wafanyakazi hao.

Kwa upande wake, Kamishna wa Chuo cha Mafunzo Zanzibar, Ali Abdalla Ali alikiri kupokea barua ya kuacha kazi kwa kijana Shaali kutokana na jazba.

“Shaali kilichomfanya aache kazi ni jazba baada ya kupelekwa Kisiwani Pemba kuendelea na kazi ya operesheni lakini alikataa”, alisema.

Alisema kwa mujibu wa sheria namba 1 ya mwaka 1980 na kufanyiwa marekebisho chini ya sheria namba 3 ya mwaka 2007 mtumishi aliyetumikia Chuo cha Mafunzo atapata kiinua mgongo baada ya kutimiza miaka 25 ya kazi kisheria na kama atastahafu chini ya umri huo atalipwa stahiki zake kwa muda aliotumikia.

Kuhusu kiinua mgongo alisema mfanyakazi anapomaliza muda wake wa utumishi huandikiwa barua na kupelekewa mkaguzi ili atayarishiwe kiinua mgongo chake muajiriwa anaestahafu na ikiwa mfanyakazi ana mkopo benki anapewa barua yake ya benki kuwa anadaiwa kiasi gani ili kukatwa kwenye kiinua mgongo chake.

Hata hivyo alisema amepokea malalamiko mengi ya Shaali kudai kuwa alikoseshwa haki ikiwemo kulazimishwa kustahafu kwa lazima kutokana na kuwa alikuwa anadaiwa katika benki ya watu wa Zanzibar PBZ na fedha hizo kukatwa kutokana na madeni yake.

Aidha Kamishna Ali aliwataka vijana kufikiria madhara ya kuacha kazi ili kuepuka migogoro inayoweza kujitokeza.