BEIJING, CHINA

WACHIMBA migodi walionasa chini ya ardhi mashariki mwa China kwa zaidi ya wiki moja baada ya mripuko kutokea kwenye mgodi wa dhahabu wamefanikiwa kutuma ujumbe kwa waokozi.

Mripuko huo ulitokea siku nane zilizopita katika mgodi karibu na mji wa Qixia wa mkoa wa mashariki wa Shandong, na kuwaacha wachimbaji 22 wakiwa wamenasa chini ya ardhi zaidi ya mita 600 kutoka lango kuu la mgodi huo.

Baada ya kipindi kirefu bila mawasiliano yoyote,waokozi waliweza kuchimba shimo hadi chini na kusema walisikia sauti za kugonga.

Wachimbaji walituma ujumbe juu wakisema 12 bado wako hai.

Ujumbe huo kwenye karatasi ulisema wanahitaji kwa dharura dawa za ubaridi, kupunguza maumivu, watu watatu wana shinikizo la damu na wanne walijeruhiwa.

Disemba mwaka jana, wachimba migodi 23 walifariki baada ya kunasa kwenye mgodi katika mji wa kusini magharibi wa Chongqing miezi michache baada ya wengine 16 kufariki baada ya kunasa chini ya ardhi katika mgodi wa makaa ya mawe mjini humo.