KAMPALA,UGANDA
IDADI kubwa ya watu waliopigwa risasi wakati wa maandamano yaliyotokea Uganda mwaka 2020 baada ya kukamatwa kwa mgombea urais Robert Kyagulanyi,walikuwa na umri kati ya miaka 14 na 30.
Karibu watu wote waliouawa walipigwa risasi na maofisa wa uslama kichwani, shingo, mbavuni, tumboni, kifua na mgongoni.
Kati ya waliouawa pia ni mlinda usalama wa mtaani aliyeajiriwa katika mpango mpya wa serikali ya Rais Museveni kuwajiri vijana na kuwapa mafunzo namna ya kusaidia maofisa wa polisi kuimarisha usalama nchini Uganda.
Kijana huyo alipigwa risasi na kamanda wa jeshi aliyemuamrisha kumpiga risasi mtu aliyekuwa akiandamana lakini akakataa kwa sababu alikuwa anamjua mtu ambaye alikuwa ameamurishwa kumuua.
Kulingana na uchunguzi uliofanywa na gazeti la Daily Monitor nchini Uganda, maofisa usalama waliovalia sare za jeshi la Uganda UPDF waliwapiga risasi na kuwaua waandamanaji hao.
Mauaji mengine yalifanywa na maofisa usalama ambao hawakuvalia sare za kazi lakini walijaa mjini Kampala na miji ya karibu kuzima maandamanoo hayo ya siku mbili.
Gazeti la Daily monitor linaripoti kwamba karibu nusu ya darzeni ya waliouawa katika maandamano hayo walikuwa wanafunzi, 11 waendesha pikipiki maarufu kama boda boda na sita watengenezaji magari.
Hadi sasa, jeshi la Uganda limesema linaendelea na uchunguzi kutambua waliohusika na mauaji hayo, bila kukubali kwamba wanajeshi wake wala maafisa wa polisi walihusika.
Karibu watu 30 waliuawa jijini Kampala na wengine zaidi ya 25 kuuawa katika miji iliyo karibu na Kampala, ya Mukono, Masaka, Luweero, Jinja, Kyotera na Rakai.