NA TATU MAKAME

WANAFUNZI 198 wanaosoma skuli ya Kidoti Mkoa wa Kaskazini Unguja, wanaendelea kusoma chini ya miti hali inayopunguza ufahamu kwa wanafunzi kutokana na uhaba wa mabanda ya kusomea.

Mwalimu Mkuu Msaidizi Msingi skuli hiyo, Sheha Ali Ali, alisema hayo huko Kidoti wakati alipozungumza na Gazeti hili mara baada ya kumalizika kwa kikao cha kamati ya skuli pamoja na walimu na wanafunzi waliosoma skuli hiyo kujadili hatua ya kuondosha tatizo hilo.

Alisema licha ya wananchi kutoa michanga yao kwa ajili ya ujenzi wa madarasa manane yenye majengo mawili, lakini hadi sasa wameshindwa kuezeka kutokana na hali ya maisha.

Alibainisha kwamba miongoni mwa hatua walizochukua ni kutafuta wafadhili na wadau wa elimu, ingawa jitihada zao zimegonga mwamba kutokana na gharama kubwa za kuezeka.

Alieleza kuwa mbali ya wanafunzi hao pia kuna wanafunzi wengine wapya 230, ambao wameandikishwa kwa ajili ya kuanza masomo kwa mwaka huu, hali inayoweza kuongeza idadi ya wanafunzi watakaoendelea kusoma chini ya miti.

Mwalimu mkuu huyo alisema changamoto nyengine walimu wengi wanaosomesha skuli hiyo wanaotoka mbali, hali inayoongeza mzigo kwa walimu wanaokaa karibu hasa kipindi cha mvua.

“Tunao vijana wengi ambao wamesomea lakini wanapokwenda kupeleka maombi walimu tunaoletewa wanatoka mbali wengine wanatoka hadi Umbuji kuja kusomesha skuli ya Kidoti, tunahisi ufaulu unapungua kwa tatizo hili maana walimu wetu wanachukua jitihada kubwa kusomesha na kuwasimamia vijana”, alisema.

Alisema hali hiyo imekuwa ikipunguza malengo yao ya kupasisha wanafunzi wote ambao wanasoma kidato cha nne kila mwaka.

“Katika skuli yetu mwalimu mmoja anasomesha vipindi 36 kwa darasa lenye wanafunzi 66 kwa wakati mmoja, hii inatupunguzia malengo maana tunajipanga vizuri kupasisha vijana wetu wote wa kidato cha nne lakini tunahisi na hili linatukwamisha”, alisema Mwalimu huyo.

Hata hivyo, aliwataka wahisani kujitokeza kutoa michango yao, ili waezeke majengo hayo ili kuondosha adha ya wanafunzi kuendelea kusoma chini ya miti.

Mwenyekiti wa kamati ya skuli ya Kidoti, Khatibu Machano Kombo, alisema wanaendelea kutafuta wafadhii watakaosaidia kuondosha tatizo hilo lakini wameshindwa.

“Tunaomba viongozi wetu wa serikali waje kutuona hali yetu na kutusaidia ili tuondoshe tatizo hili kwa wanafunzi wetu”, alisema.

Mkurugenzi Baraza la Mji Kaskazini ’A’ Unguja, Mussa Ali Makame, alisema nguvu kubwa iliyobakia wameielekeza kwenye mifuko ya Jimbo, ambayo itasaidia kupunguza tatizo hilo.

Hata hivyo alisema kwa upande wa Baraza la Mji mwaka huu hawana bajeti ya ujenzi katika skuli hiyo na kuwataka wahisani kujitokeza kuongeza nguvu zao kuchangia gharama za uezekaji ili wanafunzi wasome katika mazingira mazuri.

Skuli ya Kidoti ina zaidi ya wanafunzi 2,000 wakiwemo msingi 1,503 na sekondari 803 wenye madarasa 44 na vyumba 18.