NA KHAMIS AMANI

WANANCHI wameombwa kuunga mkono kwa vitendo wito uliotolewa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, wa kufanya usafi wa mazingira katika maeneo yao, ili mji wa Zanzibar uwe safi na salama.

Wamefahamishwa kwamba, usafi wa mazingira ni moja kati ya mambo yanayoifanya nchi kupiga hatua kubwa ya kimaendeleo, pamoja na kuondokana na maradhi mbali mbali yatokanayo na uchafu ikiwemo kipindupindu na maradhi ya miripuko.

Wito huo umetolewa na Sheha wa Shehia ya Kwahani mjini Unguja, Machano Mwadini Omar, katika zoezi la usafi wa mazingira lililofanyika katika Shehia hiyo.

Alisema, serikali ya awamu ya nane chini ya Rais Dk. Hussein Mwinyi, ametilia mkazo suala la usafi wa mazingira kutokana na maeneo mengi ya mji hayapo katika hali nzuri ya usafi wa mazingira.

Alifahamisha kwamba, usafi wa mazingira ni kitu muhimu katika ustawi wa maisha ya kila siku ya mwanadamu, hivyo kila mmoja anawajibika kwa nafasi yake kutunza mazingira yaliyomzunguka, ili kufanikisha maendeleo.

Alisema mazingira yanapokuwa safi na salama, inakuwa ni kivutio na kuondosha maradhi mbali mbali yatokanayo na uchafu, ikiwemo pia ni kivutio kwa wawekezaji wanapohitaji kuwekeza miradi yao mbali mbali ya kimaendeleo.

 “Mwekezaji yeyote hawezi kuwekeza miradi yake katika mazingira yasiyo kuwa safi na salama, hivyo jukumu letu kuhakikisha maeneo yetu yote yanayotuzunguka yanakuwa safi na salama kwa muda wote”, aliongeza.

Hali hiyo, alisema inaibebesha mzingo mkubwa serikali kwa kutafuta dawa na vifaa tiba kwa ajili ya kuwapatia matibabu waathirika, fedha ambazo zingetumika katika mipango mengine ya kimaendeleo, endapo jamii ingelichukua jitihada za kukabiliana na maradhi hayo kwa kuweka maeneo yao katika hali nzuri ya kimazingira.

Hivyo Sheha huyo alisisitiza kuwa, suala la usafi wa mazingira kama linavyosisitizwa na Rais wa Zanzibar Dk. Hussein Mwinyi, sio la kupuuzwa bali ni la kuungwa mkono na kila mmoja wetu kwa maslahi yao na taifa kwa ujumla.