NA MWANAJUMA MMANGA

TAASISI ya Milele Zanzibar Foundation, imesema itaendelea kuisaidia jamii katika kuibua miradi ya kijamii ya        Shehia ili kutatua matatizo mbalimbali yanayowakabili na kufikia hatua za kimaendeleo. 

Mratibu wa maswala ya elimu kutoka  taasisi ya Milele  Ali Bakari Amani, akizungumza katika mkutano wa kutathmini na kutatua changamoto za shehia huko Banda maji Kaskazini ‘A’ Unguja.

Alisema mipango hiyo inayowashirikisha wananchi kuelezea matatizo yanayowakabili katika shehia zao yakiwemo maswala ya elimu, afya maji na kuyatafutia ufumbuzi kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo hatua kwa hatua.

Alieleza kuwa taarifa hizo zitasaidia kujua vipaumbele vyao na kupanga mipango ya maendeleo pamoja na kustawisha shughuli za kijamii na kupunguza umasikini.

Alifahamisha kuwa katika kuanzisha miradi hiyo wamechagua sehemu za vijijini  kwa mujibu wa hali za kimaisha wanazoishi wanavijiji hao hivyo ni vyema wakaazi wa vijijini kuzitumia fursa hizo ili kijiiunua kiuchumi, kijamii, kiafya na kielimu.

Aidha amewataka kuwa wawazi katika kutoa changamoto zao ili kuweza kutatuliwa na kuondokana na umasikini nchini.

Nae Diwani wa wadi ya Kinyasini, Haji Kidawa Mkali, aliwataka Wananchi wa shehia ya banda maji kushirikiana na viongozi wao pamoja na  kuwa makini katika kuibua miradi ya kijamii ili kuweza kujiletea maendelao katika shehia zao.

Alisema iwapo  watashirikiana kwa pamoja na kuungana wataibua miradi mingi kwani maendeleo ya Banda maji yataletwa na wananchi wa shehia hiyo.

Kwa upande wake Sheha wa shehia ya Banda maji Mussa Haji Khamis, alisema lengo la mkutano huo ni kuifanya shehia yao kuwa na maendeleo endelevu.

Aidha Wameiomba taasisi ya milele kuendelea kuwasaidia wanachi katika kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili hasa maeneo ya vijijini, ili kukuza umarishaji wa shehia zao katika shughuli za kimaendeleo.