KATIKA kuelekea maadhimisho ya kilele cha maadhimisho ya Mapinduzi ya Zanzibar, yanyofanyika kila mwaka hufanyika hafla mbalimbali za uzinduzi na uwekaji wa miradi ya kimaendeleo, kichumi na kijamii katika maeneo mbalimbali ya Unguja na Pemba.

Kabla ya mradi husika kuthibitishwa kuwa utazinduliwa, kamati ya maandalizi ya sherehe za Mapinduzi hufika kwenye mradi husika na kuangalia hadhi, ubora na kiwango cha mradi huo.

Kutokana na ukubwa wa kipekee na hadhi za sherehe za Mapinduzi kwa wananchi wa Zanzibar, miradi ambayo haikukidhi viwango vya ubora kamati huiondoa kwenye ratiba ya uzinduzi ama kuekewa jiwe la msingi.

Kwa kawaida miradi inayozinduliwa ama kuekewa mawe ya msingi ni pamoja na skuli zikiwemo za msingi na sekondari, vituo vya afya, miradi ya maji safi la salama, viwanja vya michezo na burudani na kadhalika.

Kwa hakika miradi inayozinduliwa katika kipindi hichi huwa ina faida kubwa kwa jamii, kwani hulenga kuwaondolea matatizo ya msingi ikiwemo maradhi mbalimbali, elimu nakadhalika.

Kuzinduliwa kwa miradi ama kuekwa mawe ya msingi katika kipindi hichi, ni uthibitisho kwamba wananchi wa Zanzibar wanaendelea kunufaika, kutumia na kufaidi matunda ya mapinduzi.

Tunalazimika kuzieleza faida za mapinduzi kwa kinywa kipana tena bila ya kuona haya kwa sababu wapo baadhi ya watu wanajitia pambani eti hawazioni faida wala matunda ya mapinduzi.

Ndio maana tunawaelimisha wafahamu watu wa namna hiyo kwamba miradi ya uzinduzi wa skuli ambapo elimu inatolewa bure kuanzia chekechea hati ukomo wa uwezo wa mwanafunzi, hiyo ndiyo faida ya mapinduzi.

Faida nyengine ni pale unapokwenda hospitali una tatizo la kiafya daktari anakuhudumia bure, unakwenda kwenye dirisha dawa unapewa bure, uchunguzi wa maradhi kuanzia X-Ray, Ultrasound, ST-Scan na hata MRI bure, hiyo ndio faida ya mapinduzi.

Wito wetu kwa wananchi ni kwamba wajitokeze kwa wingi kwenye maeneo ambayo miradi hiyo itakuwa inazinduliwa na viongozi mbalimbali wa kitaifa, kwa sababu kwanza imejengwa kwa ajili ya jamii na sio mtu mwengine.