KWA hakika wananchi wamepata muamko mpya baada ya kuiona serikali ya awamu ya nane iliyoingia madarakani hivi karibuni ikionesha misingi ya uwajibikaji mbele ya umma.
Katika hatua kama hiyo ambayo imeambatana na mabadiliko mengi wapo watumishi wa umma walioyapokea kwa haraka mabadiliko na kuachana na utendaji wa kimazoea.
Lengo la kuachana na utendaji wa kimazoea ambao walikuwa nao kwa miaka nenda miaka rudi, ni kuhakikisha kwamba wanakwenda sambamba na kasi ya serikali ya awamu ya nane.
Hata hivyo kwa upande mwengine wapo watumishi wa umma ambao wameyapokea mabadadiliko kwa shingo uoande kwa sababu ufanyajikazi kazi mazoea una maslahi makubwa kwa upande wao.
Katika kundi hili pia wapo watumishi wanaoiangalia kasi ya serikali ya awamu ya nane iliyoambatana na mabadiliko na kuhimiza uwajibikaji itakuwa ya kudumu ama povu la soka?
Wenye mawazo ya kuangalia kasi ya povu la soda ndio maana wengine hujitolea kama mawakala kwa kuijaribu serikali ya awamu ya nane kwa kupitisha gari bandari bure bila ya kutozwa ushuru.
Wakati mwengine unaweza kujiuliza hivi jeuri za namna hii watu wanaipata wapi? Inakuwaje serikali inahimiza ukusanyaji mapato anatokea mwengine kwa ujeuri anapitisha bidhaa bila ya kutozwa ushuru.
Kama kuna watu hadi sasa wanadhani serikali ya awamu ya nane iko kwenye utani katika kurejesha nidhamu hasa kwenye masuala ya ufisadi, wizi, unadhirifu na uzembe wamekosea sana.
Kiukweli kwenye mambo haya watumishi wa umma hawapaswi kuijaribu serikali na kwamba umefika wakati wa kubadilika na kamwe wasisubiri kufifia kwa povu la soda.
Zanzibar ni tofauti kidogo na sehemu nyengine, inavyosemekana watu wengi wenye fedha nyingi (matajiri wa kutupwa), ni watumishi wa umma badala ya kuwa wafanyabishara.
Ukiwaangalia watumishi hao mishahara yao na muda waliotumikiwa serikali hailingani na ukubwa wa kipato na mali walizozikusanya. Hapa ndipo unapopata wasiwasi wamevuna wapi utajiri mkubwa walionao?
Lakini pia kama alivyosema Rais wetu Dk. Hussein Mwinyi kwamba maamuzi magumu atakayoyachukua hayalengi kumuandama mtu, hivyo hakuna haja ya kuwa na hofu.
Sisi tunaziamini sana kauli za Rais wetu na kwamba watu wasafi dhidi ya rushwa na ufisadi hawezi kuwa na hofu ya kuguswa kwenye maamuzi magumu.
Hata hivyo ukiwa na hofu ya kuguswa kwenye mchakato mzima wa maamuzi magumu, jitambue kuwa wewe si msafi na kwamba unatakiwa kuachana na mambo hayo kabla ya kukumbana na mkono wa sheria.
Lakini kwanini uwe na wasiwasi hivi sasa na maamuzi magumu? Mbona ulipozichota wakati unajua kuwa fedha unazozichota ni za umma hukuwa na woga wa aina yoyote?
Zama zimebadiliko hivyo tunapaswa kuendana kasi ya zama mpya, sote kwa pamoja twende sambamba kuiunga mkono serikali katika kurejesha nidhamu.