NA MUHAMMED KHAMIS

MWENYEKITI wa Chama cha ADC, Hamad Rashid Mohamed amesema wanaume wengi wanashindwa kuwaunga mkono wake zao katika harakati za uongozi kufuatia hofu ya kuvunjika kwa ndoa pindipo watafanikiwa kupata nafasi hizo.

Alisema licha ya uwepo wa muamko mkubwa kwa wanawake Zanzibar kuingia katika uongozi, bado wanawake wengi wanashindwa kufikia malengo kwa kile anachokiona ni kukosa hamasa kutoka kwa watu wa karibu.

Hamadi ambae pia ni waziri mstaafu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar awamu ya saba aliyasema hayo wakati alipokuwa akichangia uwasilishwaji wa rasimu ya kuwawezesha wanawake wa Zanzibar kushika nafasi mbali mbali za uongozi hafla iliyofanyika katika ukumbi wa Tamwa Tunguu wilaya ya Kati.

Alisema ipo haja kwa wanaume walio kwenye ndoa kujitathmini na kukubaliana na maamuzi ya wake zao wakiamini kuwa mwanamke kuwa kiongozi si sababu ya kuvunjika kwa ndoa.

Awali akiwasilisha rasimu yenye lengo la kuwainua wanawake Zanzibar katika nafasi za uongozi Mhadhiri kutoka Chuo kikuu cha Taifa Zanzibar (SUZA) Dk. Salum Suleiman Ali alisema licha ya jitihada zinazoendelea kufanyika bado wanawake wengi wapo nyuma katika nafasi za uongozi Zanzibar.

Hata hivyo Mhadhiri huyo alieleza kuwa kuna haja ya mabadiliko makubwa kwenye jamii na vyama vya siasa mabadiliko ambayo yatawekwa wazi ikiwezekana hata kuandikwa kwenye katiba za vyama vyote vya siasa.

Kwa upande wake Dk. Mohamed Said Dimwa alisema Zanzibar imekua na idadi kubwa ya wapiga kura wanawake kuliko wanaume lakini cha kushangaza wanawake wamekua wakikosa fursa za kuchaguliwa.

Alisema jamii ya wanawake wanapaswa kubadili mitazamo yao na kuona kuwa wanawake wenzao wanaweza kuwa viongozi na sio kuwadharau na kuona kuwa hawawezi kufanya lolote lile.

‘’Mimi binafsi mke wangu aliingia kwenye kinyang’anyiro cha Urais kupitia chama cha Mapinduzi CCM na nilikua wa kwanza kumuunga mkono kwa kuwa najua umuhimu wa wanawake kwenye uongozi’’aliongezea.

Naye Janeth Fussi ambae ni katibu mtendaji Taifa kupitia Ngome ya wanawake Chama cha ACT-Wazalendo alisema katika chaguzi mbali mbali zimekua na pirika zake lakini wanawake wanaogombea hukosa ulinzi stahiki kama wagombea.

Alisema inasikitisha sana kuona waliopewa mamlaka ya ulinzi kuwa ndio wanakua mstari wa mbele kuwadhalilisha wanawake wanaogombea kupitia nafasi mbali mbali za uongozi.

Mradi wa uwezeshaji wanawake katika nafasi za uongozi kwa kila wilaya Zanzibar ni wa miaka minne kutoka mwaka 2020 -2023  na utatekelezwa na Tamwa-Zanzibar,Zafela pamoja na Pegao chini ya ufadhili wa Ubalozi wa Norway Tanzania.