NA TATU MAKAME
MKUU wa Mkoa wa Kaskazini Unguja Ayoub Mohammed Mahmoud, amewataka wakandarasi wanaosisimamia uvunaji wa miwa katika kiwanda cha sukari Mahonda, kuhakikisha wanatoa stahiki za wafanyakazi wao kama sheria inavyoelekeza.
Akizungumza na uongozi wa kiwanda hicho, wakandarasi na wafanyakazi kiwandani hapo, wilaya ya Kaskazini ‘B’, Ayoub alisema kuwalipa stahiki zao kwa wakati kutaongeza ari ya kazi na kuwafanya wanufaike na ajira hizo.
Alisema kutowalipa mishahara au stahiki zao mbali ya kukiuka sheria za nchi, pia ni kuwakosesha haki hivyo aliwataka waajiri kuwapatia stahiki zao kuondosha malalamiko kwa wafanyakazi.
“Jitahidini kuondoa changamoto za ajira lakini muhakikishe mnawalipa kwa wakati ili wanufaike na uwepo wa kiwanda hiki katika maeneo yao,” alisema Ayoub.
Mapema wafanyakazi hao walimlalamikia Mkuu huyo wa mkoa kwamba wanafanyishwa kazi bila ya mikataba pamoja na kutokuwa na usalama wa afya zao hali inayohatarisha maisha yao wanapokuwa kazini.
Walieleza kuwa usalama wao ni mdogo wanapokuwa kazini pamoja na kucheleweshwa kwa malipo ya kazi zao hali inayowapa ugumu kuendelea na majukumu ya kuendesha vyema familia zao.
Kwa upande wa uongozi wa kiwanda hicho, walikiri kuchelewa kwa malipo ya wafanyakazi hao kwa baadhi ya siku kutokana na kuchelewa kufika kwa miwa kiwandani kutoka shambani kunakosababishwa na kunyesha kwa mvua.
Aidha waliahidi kuyafanyia kazi maagizo yaliyotolewa na mkuu huyo ili kuondoa changamoto zilizopo kati ya wafanyakazi na uongozi wa kiwanda hicho.