BANGUI, AFRIKA YA KATI

WAPINZANI katika Jamhuri ya Afrika ya Kati, wamepinga matokeo ya uchaguzi mkuu uliofanyika hivi karibuni, wakidai ulikumbwa na dosari.

Katika taarifa ya pamoja wagombea kumi wa upinzani katika uchaguzi wa rais uliofanyika Disemba 27 walitaka matokeo ya uchaguzi huo yabatilishwe.

Rais wa sasa wa Jamhuri ya Afrika ya Kati Faustin Archange Touadera alitangazwa mshindi katika uchaguzi huo.

Tume ya Uchaguzi nchini humo ilimtangaza Touadera kuwa mshindi wa uchaguzi huo kwa asilimia 53.92 ya kura zilizopigwa.

Endapo ushindi huo utathibitishwa na mahakama ya juu ya taifa hilo, itamaanisha kuwa hakutokuwepo duru ya pili ya upigaji kura.

Mgombea aliyeshika nafasi ya pili kwa kupata asilimia 21,01, waziri mkuu wa zamani Anicet Georges Dologuele, alisema tume ya uchaguzi imechukua hatua ya kuwapuuza wapiga kura karibu laki tisa na nusu (950,000) waliozuiwa kupiga kura kutokana na ghasia za makundi yenye silaha.

Mgombea aliyeshika nafasi ya tatu Martin Ziguele alisema  hayapi umuhimu wowote matokeo yaliyotangazwa na tume, aliyoyataja kuwa aibu kwa nchi.

Kwa mujibu wa mwenyekiti wa tume ya uchaguzi, karibu nusu ya waliotimiza masharti ya upigaji kura, yaani watu 910,000 walijiandikisha kwa ajili ya uchaguzi wa Desemba 27 na takriban asilimia 76.3 miongoni mwao walishiriki katika upigaji kura.

Tangu alipoingia madarakani mwaka 2016 hadi sasa Rais  Faustin-Archange Touadéra amekuwa akifanya jitihada kuhakikisha maeneo mengi makubwa ya nchi hiyo yanayoshikiliwa na makundi ya wanamgambo yanarejea kwenye udhibiti wa serikali.