NA KHAMISUU ABDALLAH
WAGONJWA wa maradhi ya presha wameshauriwa kupima afya zao mara kwa mara na kufuata ushauri wa daktari ili kuepusha madhara yakiwemo ya kupooza.
Kauli hiyo ilitolewa na Meneja wa Kitengo cha Maradhi yasioambukiza Omar Abdalla Ali, wakati akitoa elimu kwa vyombo vya habari katika ofisi za Jumuiya ya Maradhi yasioambukiza Mpendae, wilaya ya Mjini Zanzibar.
Alisema ni jambo la msingi kwa mtu anaegundulika na maradhi hayo kubadili mfumo wa maisha ikiwa ni pamoja na kupunguza kula vyakula vyenye chumvi nyingi, kufanya mazoezi na kula dawa kama walivyoshauriwa na daktari.
Aidha alisema wagonjwa wengi wamekuwa wakipata maradhi ya kupooza baadhi ya viungo vyao kutokana na kutofuata ushauri wa daktari na kula wanavyokatazwa.
Meneja Omar alisema ili kuyadhibiti maradhi yasioambukiza ambayo kwa sasa yamekuwa ni miongoni mwa maradhi yanayoongoza katika kuchangia vifo hapa Zanzibar ni vyema kwa wananchi kujikinga na vichocheo vinavyochangia maradhi hayo ikiwemo ulaji wa vyakula vyenye uwanga kwa wingi na matumizi ya sigara.
Hata hivyo aliwasisitiza wagonjwa kuacha kuchanganya dawa za hospitali na za asili kwani zinaweza kumsababishia mgonjwa presha yake kupanda na kupata maradhi ya kupooza hafla.
Akizungumzia sababu zinazopelekea ugonjwa wa presha alisema ni pamoja na ubongo kushindwa kufanya kazi kutokana na kuathirika kwa mfumo wa kusambaza damu kwenye ubongo na mishipa ya damu kuziba kutoka damu kwenye ubongo kutokana na kupasuka kwa mishipa ya damu.
Sambamba na hayo alibainisha kuwa dalili za kiharusi zinatokana na mtu kushindwa kutembea vizuri, kupata udhaifu upande mmoja wa mwili, kutoona vizuri, kupata maumivu makali ya kichwa, moyo kushindwa kufanya kazi, kuchganyikiwa na sababu nyengine.
Aliwasisitiza mama wajawazito kujitahidi wakati wa ujauzito wao kwenda vituo vya afya mapema ili kuepusha kuzaa watoto wafu na wenye kisukari.
Alifahamisha kuwa maradhi ya shinikizo la damu yana uwiano mkubwa na maradhi ya kisukari kutokana na dalili nyingi kufanana pamoja na kuwa ni maradhi sugu ambayo hayana tiba zaidi ya kupunguza kasi ya maradhi hayo.
Hivyo aliviomba vyombo vya habari kuisaidia serikali kutoa elimu juu ya kujikinga na maradhi hayo ambayo bado yanaendelea kupoteza maisha ya watu.
Kwa upande wake Meneja wa Jumuiya ya Watu Wanaoishi na Maradhi Yasioambukiza Zanzibar (ZNCD), Haji Khamis Fundi, alisema hivi sasa imebainika wananchi waliowengi wanabainika wakiwa na maradhi hayo katika hatua ya mwisho ambavyo huchangia kwa kiasi kikubwa maradhi ya kiharusi na vifo vya ghafla.