NA ASYA HASSAN

WAJASIRIAMALI na wafanyabiashara wanaoshiriki Tamasha la saba la Biashara Zanzibar wameishauri serikali kuliimarisha na kuwavutia wazalishaji na wafanyabiashara wengi.

Wakizungumza na gazeti hili kwa nyakati tofauti katika viwanja vya Maisara wilaya ya Mjini Unguja, linapofanyika tamasha hilo, walisema tamasha la mara hii ni tofauti na yaliyopita hasa katika uwekaji wa miundombinu na upangaji wa mabanda.

Walisema uwekaji wa mabanda yamepangwa vizuri lakini kuna baadhi ya changamoto ya kukosekana kwa mazulia ya kutandika chini ambapo mwaka huu limetandikwa plastiki ambalo halipo katika kiwango kizuri.

Walieleza changamoto nyengine ni wajasiriamali wadogo kuwekwa mabanda ya ndani ambapo hali ya hewa haipo vizuri na kila mjasiriamali na afya yake.

“Leo tuna siku ya pili toka kuanza kwa tamasha hili, hivyo ni vyema wakatujengea sehemu zilizobaki kwani humu ndani kama huna feni huwezi kukaa na wengine afya zetu mtihani,” walisema.

Walisema tamasha hilo ni kubwa na linashirikisha wafanyabiashara na wajasiriamali kutoka ndani na nje ya Tanzania, hivyo ni vyema kuboreshwa zaidi pamoja na kuwekewa miundombinu imara ili watu wazidi kuvutika.

Mbali na hayo walitumia fursa hiyo kuiomba Wizara ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda pale wanapoweka vikao vyao ni vyema kuwashirikisha na baadhi ya wajasiriamali hao ili waweze kutoa mapendekezo yao.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda, Juma Hassan Reli, alisema ni vyema kwa washiriki wa tamasha hilo wanapobaini kasoro katika maonyesho hayo kuziwasilisha mapema ili kuweka mipango mizuri katika tamasha hilo na mengine yanayofuatia.

Alisema serikali inafanya tamasha hilo kila mwaka ili kuwasaidia wajasiriamali hao kutangaza bidhaa zao pamoja na kupata soko la uhakika hivyo ni vyema washiriki hao kuwa wawazi ili kufanikisha malengo ya tamasha hilo.

Tamasha la saba la biashara lilianza januari 4 mwaka huu, linatarajiwa kufunguliwa rasmi leo na makamu wa rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 57 ya Mapinduzi ya Zanzibar ya Januari 12, 1964.