NA NASRA MANZI

MKUU wa Mkoa wa Kaskazini Unguja, Ayoub Muhamed Mahmoud ameitaka Jumuiya ya wazazi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) jimbo la Jang’ombe kusimamia maadili ya uongozi ili kupata misingi bora katika nchi.

Kauli hiyo ameitoa katika kongamano la jumuiya hiyo, lililofanyika   Kendwa, Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Alisema suala la maadili bora ndio misingi ya uongozi katika sehemu mbali mbali za kazi hivyo ni vyema kuunga mkono jitihada za awamu ya nane ambayo inasimamia maadili na kuondosha changamoto zilizopo na kufikia malengo iliyojiwekea.

Hata hivyo alisema moja ya changamoto ya kushuka kwa maadili katika jamii kutokana na baadhi ya viongozi, wazazi, walezi kutosimamia vyema majukumu ambayo yatawavunja moyo wananchi ambao wanawaongoza.

“Endapo viongozi, walezi na hizi jumuiya zitasimamiwa imara kwa maadili bora ya uongozi yataimarika na tutafikia yale malengo ya maendeleo katika shughuli zetu za kila siku,” alisema

Akizungumza suala la udhalilishaji, Ayoub alisema ni vyema Jumuiya kuacha muhali katika kufichua vitendo hivyo ili kupatikana taifa bora kwa vijana katika jimbo la Jang’ombe.

Akitoa mada Ofisa kutoka Wizara ya Uchumi wa blue na Uvuvi Omar Hakim Foum, alisema uchumi huo unaongozwa na serikali na taasisi binafsi kwa misingi ya wadau kuangalia njia sahihi ili kufikia mahitaji ya vizazi vya sasa na badae bila kuharibu uwezo wa maumbile ya bahari na ukanda wa pwani ili kuinua shughuli za kiuchumi na maisha bora.

Nae Mjumbe wa Kamati ya tekelezaji ya jumuiya hiyo, Salma Khairalla, akitoa mada ya udhalilishaji alisema katika kuhakikisha vitendo hivyo vya udhalilishaji vinaepukika ni vyema kurudisha malezi ya zamani kwa wazazi pamoja na kuondosha muhali katika kutoa ushahidi katika vyombo vya sheria.

Akitoa shukrani mmoja ya wanachama wa jumuiya ya wazazi Ramadhani Suleimani, alisema taaluma waliyoipata wataifanyia kazi na kuwapatia vijana na kuwa walimu bora katika jamii.