JUMA KHATIB SHAALI, JKU

NAIBU Katibu Mkuu Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Idara Maalumu za SMZ Sida Mohamed Himidi, amewataka vijana waliohitimu mafunzo katika skuli za ufundi na sekondari za JKU kuyafanyia kazi mafunzo walioyapata ili waweze kujiajiri katika fani mbalimbali zilizopo nchini.

Aliyasema hayo wakati wa sherehe za mahafali ya 11 kwa skuli ya sekondari na ya 43 kwa skuli ya ufundi yaliyofanyika katika skuli ya Sekondari JKU Mtoni, mkoa wa Mjini Magharibi.

Alisema JKU imekua mstari wa mbele katika kuhakikisha wanatoa elimu ya ufundi na sekondari kwa vijana ili kutekeleza Agizo la Rais wa awamu ya kwanza wa Zanzibar Hayati Mzee Abeid Amani Karume ambae ndie muanzilishi wa Kambi za Umoja wa Vijana hapa Zanzibar.

Hata hivyo aliwataka walimu kuwajibika ipasavyo na kuepusha ubaguzi wa namna yoyote ile ili kuendana na kasi ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Mwinyi kwa kuepuka rushwa, ubadhirifu wa mali ya umma na uzembe kazini.

Nae Mkuu wa Skuli za Sekondari JKU Mtoni, Luteni Kanali Haji Sheha Khamis, alisema jumla ya wanafunzi 765 wamehitimu masomo yao miongoni mwao 520 ni kutoka katika skuli ya ufundi na 245 kutoka katika Skuli ya Sekondari.

Akisoma Risala kwa Niaba ya wanafunzi wenzake, Abdulrahman Haji Ali, alisema kua wameweza kujifunza zaidi ya masomo 20 na kufafanua kua wamekabiliana na changamoto mbalimbali ikiwa ni pamoja na uchache wa madasa, upungufu wa walimu pamoja na ukosefu wa ajira pindi wanapomaliza masomo yao.

Sherehe za mahafali hayo zilizohudhuriwa na maofisa na wapiganaji wa jeshi hilo, ziliambatana na shamrashamra ukiwemo utenzi maalum, ngonjera pamoja na utoaji wa vyeti na zawadi kwa walimu na wanafunzi waliofanya vizuri zaidi katika masomo yao.