NA MWAJUMA JUMA

TIMU ya soka ya Kilimani City imefanikiwa kuibuka na ushindi wa bao 1-0 katika mchezo wake wa ligi daraja la Kwanza Kanda ya Unguja uliochezwa juzi.

Mchezo huo ulichezwa katika uwanja wa Amaan saa 10:00 za jioni na kushuhudiwa timu hiyo ambayo mechi yake iliyopita walifungwa na Taifa kwa idadi kama hiyo, wakifuta machungu yao hayo kwa wapinzani wao wa karibu Jang’ombe Boy’s.

Katika mchezo huo ambao pia ulishuhudiwa na makocha wao wapya kutoka Itali miamba hiyo ilionekana kucheza kwa ari zao zote ili kila mmoja kutaka kuondoka na ushindi.

City ambayo kwa sasa itakuwa na makocha wawili na wasaidizi wawili ilijipatia bao lake hilo kupitia kwa mchezaji wao Khatibu Subira Khatibu

Mbali na mchezo huo pia katika uwanja wa Mao Zedong nako kulikuwa na mchezo kati ya Mchangani United na Dula Boy’s ambao ulimalizika kwa Dula Boy’s kushinda mabao 3-1.

Dula Boy’s kupitia matokeo hayo imefanikiwa kufikisha pointi sita na kuwa nafasi ya saba ya msimamo wa ligi hiyo wakati Mchangani United inaendelea kudima katika nafasi yake ya pili kutoka mkiani ikiwa na pointi nne.

Huko katika uwanja wa Mchangani timu ya Ngome ikawatambia Mchangani FC kwa kuwafunga bao 1-0.

Kwa matokeo ya mchezo huo Kilimani city imefikisha pointi tisa na kuwa nafasi ya tatu wakati Ngome imefikisha pointi 10 na kuongoza katika msimamo wa ligi hiyo.