NA MARYAM HASSAN

VIJANA watano wamefikishwa katika mahakama ya mkoa Vuga, kwa tuhuma za kutenda kosa la kuvunja jengo mchana kwa dhamira ya kutenda kosa.

Vijana hao kwa pamoja, walipandishwa katika mahakama ya mkoa Vuga mbele ya Hakimu Salum Hassan Bakari na kusomewa mashitaka yao na wakili wa serikali, kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), Shamsi Saad.

Akitaja majina ya washitakiwa ha, wakili huyo alisema Ali Kombo Haki (23), Khalid Juma Mwalimu (29), Ali Juma Mwalimu (28), Muhsini Fuom Haji (19) na Hija Haji Hija (28), wote wakaazi wa Daraja bovu.

Alisema kosa hilo walitenda Febuari 27 mwaka jana majira ya saa 6:00 za mchana huko Monduli Darajabovu wilaya ya Magharibi ‘A’, mkoa wa Mjini Magharibi Unguja.

Washitakiwa hao kwa pamoja walivunja nyumba ya Yahya Khamis Mgosi, kwa nia ya kutenda kosa ndani humo.

Aidha alisema, baada ya kuvunja kwa pamoja walitenda kosa la wizi ndani humo na kufanikiwa kuiba redio mbili, moja aina ya rising na nyengine aina ya west.

Pia waliiba spika mbili aina ya Panasonic, power bank moja, simu aina ya Nokia, mapazia na henga vyote vikiwa na thamani ya shilingi 1,300,000 na fedha shilingi 700,000 mali ya yahya Khamis Mgosi.

Aidha katika kosa la tatu, walishitakiwa kwa kuharibu mali ya mtu, kinyume na kifungu cha 326 (1) cha sheria nambari 6 ya nmwaka 2018 sheria ya Zanzibar.

Kwa pamoja bila ya halali wanadaiwa kuharibu migomba na miwa ya Yahya Khamis Mgosi na kupelekea hasara ya shilingi 20,000 kwa makisio.

Mara baada ya kusomewa mashitaka yao kwa pamoja walikataa nakuiomba mahakama kuwapa dhamana, jambo ambalo lilikubaliwa mahakamaani hapo.

Hakimu Salum alimtaka kila mmoja asaini bondi ya shilingi 500,000 pamoja na kuwasilisha wadhamini wawili, ambao watasaini kima hicho hicho pamoja na barua ya Sheha na kopi ya kitambulisho cha Mzanzibari Mkaazi.

Pia aliahiahirisha shauri hilo hadi Januari 21 mwaka huu kwa ajili ya kuanza kusikilizwa ushahidi.