NA MARYAM SALUM, PEMBA

SHAHIDI wa kesi inayomkabili mtuhumiwa Hafidh Mahmoud Khamis, anayedaiwa kuwaingilia kinyume cha maumbile watoto wawili wa kike wa kati ya umri wa miaka sita na minane, ameithibitishia mahakama kwamba watoto hao walifanyiwa vitendo hivyo.

Shahidi huyo ambaye ni Daktari wa hospitali ya Wete,

alithibitisha hayo kwa mujibu wa uchunguzi aliowafanyia.

Akitoa ushahidi wake mbele ya Hakimu Abdalla Yahya Shamhun, alidai katika uchunguzi aliowafanyia, vipimo vilionyesha watoto hao wameingiliwa kinyume na maumbile.

Alidai kuwa waathirika hao, kwa mujibu wa uchunguzi huo, walipelekea kupata maumivu na athari  kubwa

kwenye sehemu hizo za nyuma.

Shahidi huyo alidai kuwa, kipimo ambacho alikitumia kufanyia uchunguzi zaidi kwa waathirika hao, kilionyesha majibu kwamba hawakubakwa, bali mtuhumiwa wa kitendo hicho alichukua uume wake na kuwasugulisha katika sehemu zao za mbele, kwani kulikuwa na wekundu wekundu.

Alidai kuwa, kipimo kilionyesha sehemu zao za nyuma za waathirika hao zilikuwa zipo wazi, jambo ambalo lilipelekea mmoja kati yao kutoka kinyesi ovyo kwenye sehemu ya tupu yake.

Baada ya ushahidi huo, Mwendesha Mashitaka wa mahakama hiyo Ali Amour Makame, aliiambia mahakama kuwa wanafunga ushahidi wao katika kesi hiyo.

“Mhe. kwa upande wetu tumeshamaliza kusikiliza mashahidi, hivyo  tunaiomba mahakama yako tukufu iahirishe shauri hili na kulipangia tarehe nyengine

kwa ajili ya uamuzi mdogo (rulling)”, alidai Mwendesha

Mashitaka huyo.

Hakimu Shamhun, hakuwa na pingamizi juu ya ombi la upande wa mashitaka, aliliahirisha shauri hilo hadi Februari 28 mwaka huu kwa ajili ya uamuzi mdogo.

Mshitakiwa wa kesi hiyo anakabiliwa na makosa manne, ambayo aliyatenda kwa nyakati tofauti kwa waathirika hao.

Kosa la kwanza ilidaiwa ni la kubaka, ambalo alilitenda Oktoba 9 mwaka jana majira ya saa 7:00 za mchana, huko Chanjaani Bule Wilaya ya Micheweni Pemba.

Ilidaiwa kuwa siku hiyo mshitakiwa huyo alimbaka mtoto mwenye umri wa miaka 6 (jina limehifadhiwa), jambo ambalo ni kosa kisheria, chini ya kifungu cha 108 (1) (2) (e) cha sheria nambari 6 ya mwaka 2018 sheria za Zanzibar.

Kosa la pili ilidaiwa kuwa siku hiyo hiyo baada ya kitendo hicho, pia alidaiwa kumwingilia kinyume na maumbile, kinyume na kifungu cha 133 (a) cha sheria nambari 6 ya mwaka 2018 sheria za Zanzibar.

Kosa la tatu ilidaiwa kuwa, siku hiyo hiyo alimbaka mtoto mwenye miaka 8 (jina limehifadhiwa), kitendo ambacho ni kosa na ni kinyume na kifungu cha 133 (a) cha sheria nambari 6 ya mwaka 2018.

Kosa la nne kwa mshitakiwa huyo ilidaiwa kuwa, siku hiyo hiyo baada ya kitendo hicho, alimwingilia muathirika huyo kinyume na maumbile, jambo ambalo ni kosa kisheria.