NA ASIA MWALIM

TAASISI ya Korean Cultural for Foundation, imewataka wadau na watu wenye uwezo kuwasaidia watoto wagonjwa na wasio jiweza kimaisha, ili kukidhi mahitaji yao ya kila siku.

Msimamizi wa Tasisi hiyo, Jeong Yeon Sook, alitoa wito huo wakati akikabidhi vifaa mbalimbali kwa watoto waliolazwa huko hospitali ya Mnazimmoja Mjini Zanzibar.

Alisema watoto wanahitaji faraja hasa wanapokua na wakati mgumu, hivyo taasisi hiyo imeamua kutoa msaada huo kama ni faraja kwa watoto waliolazwa hospitalini hapo.

Aidha, alisema kutoa misaada kunamarisha maisha ya wanyonge ambao wanaishi katika hali ngumu sambamba na kuleta maendeleo ya wazanzibari.

Alifahamisha kuwa lengo la kutoa msaada huo hospitalini hapo ni kuwafariji watoto ambao hawawezi kujumuika na wenzao walipo nje kwenye kushereheka, hivyo vifaa hivyo vitawapa furaha.

Alieleza kuwa kampuni hiyo hutoa misaada yake inapofika kipindi cha Skukuu ya Krismas, kwa mwaka huu wamelazimika kuchelewa kutokana na janga la Corona.

“Mwaka uliopita nilitoa zawadi kipindi cha sherehe kwa watoto waliolazwa hospitali ili wapate faraja kama watoto wengine waliopo majumbani ingawa mwaka huu Corona imetuchelewesha” alisema. 

Alisema Taasisi hiyo ina angali maslahi ya watoto zaidi ambao ndio tegemo la baadae na aliwashukuru viongozi wa Serikali kwa mashirikiano yo na kuweza kufanikisha msaada huo sambamba na kuhakikisha msaada huo umewafikia walengwa.

Hafidh Ali Ramadh Diwani wa Wadi ya Mbweni, alisema wameishauri kampuni hiyo kuanza na msaada hospitali kuu ya Mnazimmoja kwani wagonjwa wa maeneo mengi hufika hapo.

Aidha aliwataka wafadhili wanaotoa misaada mitaani washirikiane na viongozi wa Serikali ikiwemo masheha, madiwani ili waweze kuwapa utaratibu unaofaa.

Diwani wa Mombasa ambae ni Mwenyekiti wa Madiwani Wiaya ya Magharibi ‘B’ Maulid Mwinjuma Mzee, alisema viongozi wanajukumu la kusimamia wadau wanatoa misaada hivyo wameamua kushirikiana na taasisi hiyo ilyotoka nje ya nchi.

Hata hivyo aliwataka watu walio karibu na watu wenye uwezo wawashajihishe kutoa misaada itakayoleta maedeleo katika jamii.

Nao waliopokea msaada huo walishukuru taasisi hiyo kwa kuwapa vifaa hivyo ambavyo vitawasaidia katika masomo, mavazi pia kuwaomba wafadhili wengine kujitokeza kuwasaidia wanyonge ili kutatua changamto zao.

Taasisi hiyo chini ya usimamizi wa Korea imekabidhi msaada wa vitu mbalimbali vyenye thamani ya shilingi 2,100,000. ikiwemo vifaa vya skuli, vyakula, vitu vya kuchezea.