NA KHAMIS MOHAMMED

JUMLA ya watu 180 wamefariki katika ajali 306 zilizotokea mwaka 2020 huku zikiacha majeruhi 372 visiwani hapa.

Hayo yamebainishwa na Mtakwimu Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Asha Mussa Mahfoudh, alipokuwa akiwasilisha ripoti ya takwimu za ajali na makosa ya barabarani jana.

Alisema, kwenye ajali hizo kulikuwa na waathiriwa 552 ambao kati ya hao 469 walikuwa wanaume sawa na asilimia 85 na wanawake ni 83 sawa na asilimia 15.

Alisema, wilaya ya Magharibi ‘A’ imeripotiwa kuwa na ajali nyingi ambazo zilikuwa 74, ikifuatiwa na Mjini ajali 46 na Magharibi ‘B’ ajali 42.

Alisema jumla ya waathirika wa ajali za barabarani waliojeruhiwa na waliokufa, abiria ni 220, wapanda baiskeli na pikipiki ni 189, watembea kwa miguu 110 na madereva 33.

Alisema, ajali zilizoripotiwa mwaka 2020 zimeongezeka kutoka ajali 301 mwaka 2019 hadi 306 mwaka 2020 kwa asilimia 1.7 wakati idadi ya waathirika imepungua kwa asilimia 0.7.

“Mwaka 2019 kulikuwa na waathirika 556 na mwaka 2020 ni waathirika 552”, alisema.

Kwa upande wa makosa ya barabarani yalikuwa 19,003 mwaka 2020 ambapo makosa 18,985 yalifanywa na wanaume sawa na asilimia 99 na makosa 18 yalifanywa na wanawake.

Alisema, kutofuata miongozo na kanuni za usalama barabarani lilikuwa kosa kuu, makosa 4,674 ambapo wilaya ya Mjini iliongoza ikiwa na makosa 3,396 sawa na asilimia 17.9 huku Micheweni ikiwa na idadi ndogo ya makosa 410 (asilimia 2.2).

Juu ya ajali za barabarani kwa mwezi Disemba 2020, ziliripotiwa ajali 26, zikiwa zimeongezeka kwa asilimia 23.8 kutoka ajali 21 mwezi Novemba.

Mkuu wa Kitengo cha Takwimu za Makosa ya Uhalifu Makao Makuu ya Polisi Zanzibar, Mkaguzi Msaidizi wa Polisi, Khamis Mwinyi Bakari, alisema, jeshi la polisi kwa kushirikiana na Mamlaka ya Usafiri na Usalama Barabarani, linaendelea na operesheni mbalimbali katika kukabiliana na madereva wanaosababisha ajali.

Aidha, alisema, kiasi cha shilingi zaidi ya milioni 196 zilipatikana ikiwa ni tozo zilizolipwa mahakamani kwa makosa mbalimbali ya barabarani mwaka 2020.

Naye Ofisa Kitengo cha Usalama Barabarani Makao Makuu ya Jeshi la Polisi, Koplo Ali Abdalla Juma, alisema, wameandaa mikakati ya kupunguza ajali barabarani kwa kuwabana madereva watakaosababisha ajali ikiwemo kufanya upya mitihani ya darasani na vitendo.

“Tutazuia leseni yake na kuipeleka mamlaka husika kwa ajili ya kuhakikiwa kwa mitihani na sheria za barabarani kwa vitendo”.

“Hii inaweza ikasaidia kwa madereva ambao watakuwa wamesahau au kwa makusudi sheria za usalama barabarani”.

“Lakini pia tutaendelea kufanya operesheni kwa kushirikiana na vikosi vyengine ili kudhibiti ajali na baadhi ya makosa ya barabarani na kuhakikisha wananchi wanakuwa katika hali ya usalama”.