NA TATU MAKAME

ZAIDI ya wanakisomo cha watu wazima 800 wanatarajia kuanza mitihani yao Januari 25 mwaka huu, ili kupima uwezo wao kupitia vituo mbalimbali Unguja na Pemba.

Akizungumza na Walimu na waratibu wa elimu, Raha leo Wilaya ya Mjini Unguja, Mkurugenzi wa elimu Mbadala na watu wazima, Mashavu Ahmada Fakihi, alisema lengo la kufanya mitihani hiyo ni kupima uwezo walionao wanafunzi wa kusoma na kuandika.

Mashavu alisema mitihani hiyo itaweza kuwasaidia wanafunzi kujua hatua waliyofikia na uwezo walionao katika kufanya mitihani pamoja na kujua idadi ya wanakisomo watakaofanya mitihani hiyo.

Hata hivyo, aliwataka walimu na waratibu kusimamia vyema wanafunzi hao ili kuepusha udanganyifu.

 “Ni vyema wasimamizi na waratibu mukasimamia vyema ili wanafunzi hao kujiepusha na udanganyifu kwani

tunatumia fedha nyingi kutunga mitihani ”, alisema.

Nae Mratibu wa Kituo cha Elimu Mbadala na Watu Wazima Wilaya ya Kati, Issa Suleiman Saleh, aliwataka waratibu kufuatilia wanavisomo wao, ili kujua changamoto zao.

Nao wanafunzi wanaotarajia kufanya mitihani hiyo walisema wamejipanga vyema kufanya mitihani yao na matarajio yao kufanya vizuri ili kujua uwezo wao wa kusoma na kuandika.

Mitihani hiyo ambayo hufanywa kila mwaka itasaidia kujua maendeleo ya wanafunzi wanaosoma katika madarasa ya watu wazima katika vituo mbalimbali Unguja na Pemba.