NA MWANDISHI WETU

NI hapo juzi Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk Hussein Ali Mwinyi alipowataka viongozi wa majimbo kuwa karibu na wapiga kura wao.

Kauli ya Rais Mwinyi ni kuwakumbusha tu wajibu wao viongozi hao wa majimbo ambapo wengi wao baada ya kuchaguoliwa kwenye uchaguzi mkuu huwa hawapiti tena majimboni mwao hadi wakati wa kuomba kura.

Hali kama hii inawaacha na butwaa wananchi hasa kwa kuwa viongozi hao hupita nyumba kwa nyumba kuomba kura na ahadi teletele.

Ni ukweli usiopingika kuwa hii inatokana kuwa ndani ya majimbo kumekuwa na changamoto nyingi zinazowapata wananchi, na sehemu pekee ya kuziwasilisha ni ndani ya chombo hicho ambacho kipo kwa ajili ya kuangalia maisha yao yanavyokwenda, na namna ya serikali itavyoweza kuyapatia ufumbuzi.

Hivyo, kauli ya rais itawafanya waajumbe wa Baraza la Wawakilishi, kutoa matumaini makubwa kwamba kutekeleza ilani ya chama cha Mapinduzi na kuleta maendeleo yaliyokusudiwa sambamba na kubuni fursa za kimaendeleo kwa wapiga kura wao.

Sambamba na hilo, lakini kumebainika kuwa wapo baadhi ya wajumbe wamekuwa hawazungumzi chochote wawapo bungeni ama baraza la wawakilishi jambo ambalo linawavunja moyo hata wapiga kura wao hasa ikizingatiwa kuwa wao ndio wasemaji wao.

Wakati wa ufunguzi wa bunge la Jamhuri ya muungano mwishoni mwa mwaka uliomaliza, Spika wa Bunge hilo, Job Ndugai, aliwaeleza wazi kuwa kukaa kimnya ndani ya chombo hicho sio kama unaisaidia serikali kwa kuonyesha ndio unaipenda, jambo ambalo ni sawa na kuiumiza.

Ni ukweli usiopingika kuwa baadhi ya Wabunge wameweka rikodi mbaya ya kutozungumza ndani ya kipindi cha miaka mitano iliyopita kiasi ambacho wananchi waliowachangua walijuta kwa nini walifanya hivyo.

Kutokana na ukweli huo, nafikiri umefika wakati kwa Wajumbe wa Baraza wakaanza kujitathmini namna ya utendaji wa kazi wanazozifanya katika Baraza hilo kama kweli wapo kwa ajili ya kuwasaidia wananchi ama wapo kwa kuangalia neema watazozipata.