NA ABOUD MAHMOUD

WAWEKEZAJI nchini wameshauriwa kupanga mikakati itakayohakikisha lengo la kuhifadhi mazingira linafikiwa.

Ushauri huo umetolewa na Mwenyekiti wa Baraza la Mji Kati, Said Hassan Shaaban, wakati alipofanya mazungumzo na wawekezaji wa mahoteli, wananchi na wanakamati za mazingira katika ukumbi wa MACEMP, uliopo Uroa wilaya ya Kati Unguja.

Mwenyekiti huyo alisema kupanga mikakati hiyo kutasaidia kuimarisha usafi wa fukwe za hoteli hizo pamoja na vijiji vilivyokuwemo ndani ya ghuba ya Uroa.

“Napenda kutoa ushauri kwa wamiliki wa hoteli, wanakijiji wa Uroa na wanakamati za mazingira, wote kwa pamoja muhakikishe mnaweka mikakati ili kuhakikisha mnahifadhi mazingira ya maeneo yenu,” alisema.

Mwenyekiti huyo ambae pia ni Diwani wa kuteuliwa alisema ipo haja kwa wamiliki wa hoteli kuhakikisha wanashirikiana na jamii katika kuleta maendeleo na kutatua matatizo yanayowakabili.

Alisema ushirikiano wao huo utaweza kuibua mambo mbali mbali ikiwemo kutatua changamoto pamoja na kuleta maendeleo ambayo wananchi wengi wanayahitaji.

Naye Diwani wa wadi ya Chwaka, Mlenge Khatib Mlenge, alisema suala la usafi ni muhimu kwani licha ya kutiliwa mkazo na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi, lakini pia huimarisha afya kwa wananchi jambo ambalo ni muhimili wa maisha ya kila siku.

Hivyo aliwataka wananchi pamoja na wamiliki wa hoteli zilizomo ndani ya kijiji cha Uroa kuhakikisha wanadumisa usafi ndani na nje ya maeneo yao ili kujiweka salama na kujiepusha na maradhi mbali mbali.