NA JARIA ABDI

MENEJA Mkuu wa hoteli ya Pemba Paradise, Hassan Othman iliyoko Makangale Mkoa wa Kaskazini Pemba, ameiomba serikali kuimarisha miundombinu ya barabara ili kufutia watalii katika hoteli yao.

Alisema hayo wakati  akizungumza na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Uchumi na Uwekezaji, Mudrik Ramadhani Soraga, alipofika kuangalia maendeleo ya uwekezaji.

Alisema miundombinu ya barabara kutoka hifadhi ya msitu wa Ngenzi mpaka hadi Makangale ni tatizo kubwa hasa kipindi cha mvua na hivyo kusababishwa watalii kushindwa kufikia hotelini pao.

“Kuwepo eneo la hifadhi la msitu huo sio sababu ya barabara hii kutojengwa, tunaiomba serikali iangalie uwezekano wa kuijenga ili ipitike wakati wakati wote,” alisema.

Alitolea mfano msitu wa Jozani akisema kwamba haikuwa kizuizi kwa serikali kujenga barabara hiyo licha ya kuwa msitu huo ni hifadhi muhimu.

Nae mwekezaji Hassan Juma Ali kutoka Fundo wilaya ya Wete, alisema, kilichomvutia kuwekeza katika kisiwa hicho ni  mandhari yake na kuwepo vivutio vingi vya utalii.

Alisema kama kisiwa hicho kitatumiwa vizuri kinaweza kusaidia kuiingizia serikali kiwango kikubwa cha fedha.


Akizungumzia changamoto zinazomkabili alisema ni pamoja na  vitendo vya hujma vinavyofanywa na wananchi wasiojuilikana.

Alisema watu hao huchoma moto mara kwa mara na
kurudisha nyuma shughuli za uwekezaji.“Eneo hilo nimelipata tangu mwaka 2007 kwa kupitia taratibu zote za serikali pamoja na vibali vya kumiliki eneo na 2014 nikaanza rasmi ujenzi huo, matumaini yangu ilikuwa baada ya miezi mitatu ni kufungua mahawa baada ya kumaliza matengenezo lakini haikuwezekana baada ya kuchomwa moto na watu wasiojulikana,” alisema.