NA KHAMISUU ABDALLAH

VIJANA wawili waliodaiwa kuiba simu yenye thamani ya shilingi 230,000 wamefikishwa katika mahakama ya mwanzo Mwanakwerekwe, kujibu tuhuma hizo.

Washitakiwa hao ni Juma Suleiman Juma (26) mkaazi wa Bububu na Ali Ramadhan Juma (27) mkaazi wa Masingini wilaya ya Magharibi ‘A’ Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja.

Wote kwa pamoja walifikishwa katika mahakama ya Hakimu Mohammed Ali Haji na kusomewa shitaka la wizi na Mwendesha Mashitaka, Koplo wa Polisi Salum Ali.

Ilidaiwa mahakamani hapo kuwa, washitakiwa hao wote kwa pamoja walipatikana na kosa la wizi, kinyume na kifungu cha 251 (1) (2) (a) na 258 cha sheria namba 6 ya mwaka 2018 sheria za Zanzibar.

Koplo Salum alidai kuwa Septemba 16 mwaka huu saa 1:30 asubuhi huko Magereza Miembeni wilaya ya Mjini Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja, kwa pamoja waliiba simu aina ya Infinix rangi ya bluu ikiwa na thamani ya shilingi 230,000 mali ya Sita Joseph Paul, kitendo ambacho ni kosa kisheria.

Washitakiwa hao waliposomewa shitaka hilo walilikataa na kuiomba mahakama iwapatie dhamana, huku upande wa mashitaka ukidai kuwa upelelezi wake tayari umeshakamilika.

Akizungumzia suala la kupatiwa dhamana washitakiwa hao, Koplo Salum alisema hana pingamizi ikiwa washitakiwa hao watafika mahakamani hapo kila tarehe wanayopangiwa.

Hakimu Mohammed alisema dhamana ya washitakiwa hao ipo wazi ikiwa kila mmoja atajidhamini mwenyewe kwa shilingi 100,000 za maandishi na kila mmoja awasilishe mdhamini mmoja, atakaemdhamini kwa kima hicho hicho cha fedha za maandishi na barua za Sheha zinazoonesha picha zao.

Mahakama iliiahirisha kesi hiyo hadi Januari 13 mwaka huu na kuamuru upande wa mashitaka kuwasilisha mashahidi siku hiyo.

Washitakiwa hao walikamilisha masharti hayo na wapo nje hadi tarehe nyengine waliyopangiwa mahakamani hapo.