NA HAJI NASSOR
WATU zaidi ya 100 wamejitokeza kuomba kumlea mtoto mchanga alietupwa na mama yake muda mfupi baada ya kuzaliwa.
Mtoto aliokotwa akiwa ametupwa pembezoni mwa ufukwe katika bahari ya kijiji cha Kwasanani shehia ya Jombwe wilaya ya Mkoani Machi 24 mwaka jana.
Hayo yalielezwa na Ofisa wa idara ya ustawi wa jamii, hifadhi ya mtoto wilaya ya Mkoani, Aisha Abdi Juma, alipokuwa akizungumza na wananchi wa shehia ya Kengeja katika mkutano wa wazi uliojadilimpango wa malezi.
Alisema suala la kutupa mtoto ni kosa la jinai, hivyo sio busara kwa jamii kuwatenga wanaobeba mimba nje ya ndoa.
Alieleza kuwa, wapo wanaotafuta watoto hata kwa dawa na ndio sababu walijitokeza wazazi 100 wakiomba kumleta mtoto huyo.
“Jamani tuhakikishe tunaelimishana juu ya madhara ya kutupa watoto kwani ni kosa la jinai kumtupa mtoto,” alisema.
Ofisa wa wanawake na watoto wilaya ya Mkoani, Asiya Abdalla, alisema moja ya sifa ya mlezi ambae anaweza kupewa mtoto na serikali ni kuwa na maadili.
Awali akizungumza katika mkutano huo, sheha wa shehia ya Kengeja, Mohamed Kassim, alisema elimu hiyo ni vyema jamii wakawafikishia wenzao.