NA KHAMISUU ABDALLAH

WAZIRI wa Uchumi wa Buluu na Uvuvi, Abdalla Hussein Kombo, amesema serikali ya awamu ya nane imetoa kipaumbele katika ufugaji wa mazao ya baharini ikiwemo majongoo ili kutoa ajira kwa vijana.

Kauli hiyo aliitoa wakati akifungua mafunzo ya siku moja uliowashirikisha wananchi mbalimbali na taasisi za kijamii wenye lengo la kuwapa elimu juu ya uchumi wa buluu na ufugaji majongoo uliofanyika katika ukumbi wa Malaria Mwanakwerekwe.

Alisema lengo la serikali kuanzisha sekta hiyo ni kuinua maisha na kukuza uchumi wa wananchi na jamii kwa ujumla.

Alisema ufugaji wa mazao ya baharini na maeneo ya hifadhi za bahari utakuwa na mchango mkubwa katika kuinua maisha ya wazanzibari kama ilivyoanishwa katika ukurasa wa 187 wa ilani ya CCM katika kutoa ajira 300,000 kupitia sekta hiyo.

Hata hivyo, alibainisha kuwa katika kufikia azma hiyo sekta binafsi zina mchango mkubwa wa kuhakikisha ufugaji na biashara ya mazao ya baharini vinaimarika na kuleta tija kwa jamii na taifa kwa ujumla.

Alisema Taasisi ya Mimi na Mwinyi ni miongoni mwa asasi za kijamii zinazodhamiria kuteleleza azma ya serikali ya awamu ya nane hivyo aliahidi kuwa wizara yake itahakikisha inatoa mashirikiano kwa taasisi zote na makundi ya vijana yanayojishughulisha katika kuendeleza shughuli za uvuvi.

Hivyo aliwasisitiza wananchi wa Zanzibar kuchangamkia fursa zilizokuwepo katika uchumi wa buluu ili kuweza kujipatia kipato na kuondokana na umasikini.

Aliwaomba wananchi wa Zanzibar kuona umuhimu wa kuhifadhi mazingira ya bahari na ukanda wa pwani huku akiwasisitiza wavuvi kuacha mara moja kutumia zana na nyenzo zenye kuharibu mazingira ya bahari.

Akitoa maelezo mafupi ya Taasisi ya Mimi na Mwinyi, Mkurugenzi Mkuu wa taasisi hiyo Salmin Botea, alisema una lengo la kuifahamisha jamii dhana nzima ya uchumi huo na fursa zilizokuwepo ili wananchi hasa vijana waweze kuzitumia.

Alisema suala la kuelimisha wananchi katika suala hilo sio la serikali pekee ndipo taasisi hiyo ilipoona umuhimu wa kutoa mafunzo hayo kwa vijana hasa katika ufugaji wa majongoo ambao ni fursa na ajira yenye kipato cha uhakika.

“Dk. Mwinyi hajafanya makosa kuchagua sera ya uchumi wa buluu kwani ni sekta yenye fursa kubwa na utajiri wa kutosha vijana ni wakati wetu kutumia fursa hizi,” alisema. 

Aidha alisema katika kuona wananchi wanafahamu uchumi wa buluu kwa upana zaidi taasisi hiyo itashirikiana na wizara katika kuandaa kongamano maalum la kumpongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi kwa dhamira yake ya kuanzisha sekta hiyo ambayo ina manufaa makubwa kwa wananchi wa Zanzibar.

Naye mkufunzi kutoka idara ya Maendeleo ya Uvuvi, Semeni Mohammed Salum alisema ni wakati sasa vijana kuamka na kumuunga mkono Dk. Mwinyi katika kuona uchumi wa buluu unaleta manufaa makubwa kwa uchumi wa Zanzibar.

Mafunzo hayo yameandaliwa na taasisi na Mimi na Mwinyi mada mbalimbali ziliwasilishwa ikiwemo dhana ya uchumi wa buluu na fursa zilizokuwepo na elimu ya ufugaji wa majongoo.