NA KIJA ELIAS, MWANGA
RAIS Dk. John Magufuli anatarajiwa kuwa mgeni rasmi kwenye uzinduzi wa mradi mkubwa wa maji wa Mwanga-Same-Korogwe, unaotekelezwa mkoani Kilimanjaro, utakapokamilika mwishoni mwa mwaka huu.
Hayo yameelezwa jana na Waziri wa Maji Jumaa Aweso, wakati wa hafla ya kuikabidhi kampuni ya hapa nchini ya Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) iliyofanyika mjini Mwanga, mkoani Kilimanjaro.
DAWASA imekadhiwa jukumu hiyo baada ya Serikali Disemba, mwaka jana, kuvunja mkataba na mkandarasi aliekuwa amepewa jukumu la kutekeleza mradi huo kufuatia kususua kwa utekelezaji wake.
Akiongea na wananchi waliohudhuria hafla hiyo, Waziri Aweso, alisema kusua kwa utekelezaji wa mradi huo umemsononesha sana Rais pamoja na viongozi wengine wakuu wa Serikali wakiwemo Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Majaliwa.
“Hata wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu wa mwaka jana, Rais Magufuli hakuacha kuizungumzia kero ambayo inawapata wananchi wa Mwanga, Same na Korogwe na ndiyo maana tukachukua uamuzi mugumu wa kusitisha mkataba na mkandarasi aliekuweko punde nilipochukua wadhifa wa Wizara ya Maji”, alisema.
Alisema kuwa yeye na uongozi mzima wa Wizara yake hatakubali kuwa kikwazo kwa wananchi wa maeneo hayo kukosa maji safi na salama na kwamba pia hawatakuwa tayari kumkwaza Rais ambaye amewaamini na katika wizara hiyo.
“Ndiyo maana nimesema ya kuwa baada ya DAWASA kutuhakikishia watakamilisha mradi huo ifikapo Novemba, mwaka huu, mtu sahihi ambaye atastahili kuuzindua mradi huu mkubwa ni Rais Dk. Magufuli na hii ni kutokana na ukubwa wa mradi wenyewe pamoja na umuhimu wake ambao ni kuhudumia zaidi ya watu 400,000 utakapokamilika”, alisema.
“Maji ni kichocheo kikubwa cha uchumi wa mtu mmoja mmoja na jamii kwa ujumla, pia muhimu sana kwa kulinda afya zetu na mazingira hivyo naahidi tutafanya kazi usiku na mchana kuhakikisha mradi huu unakamilika kwa manufaa ya wananchi na Taifa kwa ujumla”, alisema.
Alionegza, “Kukosekana kwa maji ya uhakika kwa wananchi wa Mwanga, Same na Korogwe ambao ndiyo walenngwa wakuu wa mradi huu kumechangia kuzorota kwa shughuli za Maendeleo yenu na ndiyo maana Serikali imeaumua kubadilisha mfumo wa utekelezaji wa mradi huu mkubwa ili uweze kukamilika na utoe huduma kwa wananchi”.
Aidha Waziri Aweso alimuagiza Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji Mhandisi Anthony Sanga, kuhakikisha wizara inakamilisha taratibu zote za kisheria na za manunuzi ili kuepusha Serikali kuingia katika migogoro ya kimkataba na wakandarasi walioshindwa kutekeleza makubaliano ya kimkataba yanayohusiana na mradi huo.
Kuhusu DAWASA kukabidhiwa mradi huo, Waziri Aweso alisema Serikali imeamua kutoa nafasi hiyo kwa makampuni ya kizawa ambapo alisema tayari mamlaka hiyo imeonyesha mafanikio katika utendaji wake ikiwemo upatikanaji wa maji safi na salama maeneo ya Kisarawe na Mkuranga, mkoani Pwani, maeneo ambayo alisema yalikuwa hayana huduma hiyo tangu nchi ipate uhuru wake miaka 60 iliyopita.
Mtendaji Mkuu wa DAWASA Mhandisi Cyprian Luhemeja, aliahidi ya kuwa mradi huo unatarajiwa kukamilika Novemba, mwaka huu, tayari kwa makabidhiano.
“Leo Januari 19, 2021, tunakuahidi mradi huu mimi ni timu yangu tutaukamilisha Novemba, mwaka huu, panapo majaliwa na tutakukabidhi rasmi tayari kwa ajili ya uzinduzi wake Desemba 19, mwaka huu, eneo ambalo mamlaka husika itaona panafaa kwa uzinduzi huo”, alisema Luhemeja.
Akiongea katika hafla hiyo kwa niaba ya Wakuu wa Wilaya zinazopitiwa na mradi huo, Mkuu wa Wilaya ya Same Rosemary Senyamule, aliipongeza Serikali kwa uamuzi wake wa kutumia wakandarasi wa hapa nchini ambapo alielezea matumaini yake utakamilika kama inavyotarajiwa.
“Uamuzi wa Serikali unaotekelezwa leo hapa pamoja na kukamilika kwa mradi huu kama ilivyoelezwa hapa kutatoa majibu ambayo wananchi wa Same na wilaya za Mwanga na Korogwe ambayo wamejiuliza kwa muda mrefu kutokana na changamoto zinazowakabili kwa kukosa huduma ya maji”, alisema.