NA MWANAJUMA MMANGA

WIZARA ya Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo,  imesema haitomvumilia mwananchi yoyote anaekwenda kinyume na sheria za ukataji miti kiholela hasa miti ya asili. 

Waziri wa Wizara hiyo, Soud  Nahoda Hassan, aliyasema hayo huko Shakani Wilaya ya Magharib ‘B’ Unguja, kufuatia mwananchi mmoja kukata mti wa aina ya mbuyu huko shakani kinyume na sheria na kushindwa kuchukua taratibu zilizopo za ukataji wa miti.

Alisema kitendo hicho hakikubaliki kwani kinaleta uharibifu wa mazingira na kwamba hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yake.

Alisema kuwa miti ya aina hiyo kwa hapa Zanzibar ni tunu na hifadhi kubwa Hivyo iwapo wananchi wataihujumu sio tu kwamba wanaikomoa serikali bali na wananchi kwa ujumla kwani inawasaidia katika matumizi mengi. 

Aidha, Hassan aliwataka wananchi kutoa ushirikiano kwa kutoa taarifa endapo watahisi kuna uharibifu wa mazingira katika maeneo yao kabla hayajaleta athari, ili kuona miti asili na mazingira yanalindwa ipasavyo. 

Nae Kaimu Mkurugenzi Idara ya Misitu na Maliasili Zisizorejesheka, Sheha Idrisa Hamdani, alisema miti aina mibuyu imehifadhiwa kwa mujibu wa sheria naomba 10 ya misitu ya mwaka 1996, ambayo haitakiwi kukatwa bila kufuata taratibu Hivyo kosa hilo kubwa kwa sheria za Zanzibar. 

Hivyo alisema muhusika aliefanya hilo atafikishwa katika vyombo vya sheria na kuomba ushirikiano wa hali ya juu katika vyombo husika, ili kuzuia uhalifu kabla haujatokea.

Alifahamisha kuwa wataendelea kushirikiana na shehia katika masuala hayo ili kuhakikisha Zanzibar inabakia salaama na katika haiba yake. 

Sheha wa shehia ya Shakani, Mwanaisha Khamis Rashid, alisema  anasikitishwa na kitendo cha watu kufanya hujuma hiyo  cha kukata mbuyu maeneo hayo bila ya kufuata sheria za serikali iliyoekwa. 

“Nasikitishwa mimi napita kila wakati na hapo ni njiani cha kusangaza mita tatu tu baina ya mbuyu na njia na halafu umekuwa ukikatwa kimya kimya na chini kwa chini jambo ambalo linaonesha uhalifu kama huo sio mzuri” alisema sheha huyo.

Alisema yeye amepokea taarifa kutoka kwa watu wa misitu kuwa kuna mbuyu umekatwa na haujafata sheria ambao ni wa miaka mingi na ametoa wito kwa wananchi kutoa taarifa wanapoona mambo kama hayo.

Alisema hivi sasa uongizi wa shehiya pamoja na sheha wamepanga mikakati imara na kamati ya  ulinzi na usalama ili kuhakikisha wakiona mtu anaharibu mazingira  na hana kibali hatua kali atachukuliwa dhidi yao.