NA MARYAM HASSAN

WAZIRI wa Uchumi wa Buluu na Maendeleo ya Uvuvi, Abdalla Hussein Kombo, amesema wizara hiyo mpya inakabiliwa na uhaba wa wataalamu hasa katika sekta ya uchumi wa buluu.

Waziri huyo aliyasema hayo wakati akifungua kongamano lililowashirikisha wadau mbali mbali wa maendeleo katika viwanja vya maonyesho Maisara.

Alisema uhaba huo wa wataalamu si wa Zanzibar pekee bali hata kwa nchi zote ambazo zina mikakati ya kuimarisha uchumi kupitia sekta ya uvuvi.

“Sekta hii ni mpya si kwa Zanzibar tu bali hata kwenye nchi nyengine wataalam katika sekta ya uchumi wa buluu ni wachache mno”, alisema.

Alisema ili kufikia azma ya Zanzibar kuwa ya uchumi wa buluu lazima kusimamiwa vyema vipaumbele vilivyowekwa na serikali ya awamu ya nane kwa kuwepo mashirikiano baina ya serikali na sekta binafsi na wadau wa maendeleo.

Aliongeza kuwa dhana ya uchumi wa buluu kimsingi inafunganisha sekta mbali mbali za uchumi wa bahari huku akitaja miongoni mwa sekta hizo ni pamoja na uvuvi, ufugaji wa baharini wa samaki, ujenzi wa viwanda vya kusindika samaki, ukulima wa mwani, bandari na usafiri wa baharini.

Pia alisema suala la utafutaji na uchimbaji wa mafuta na gesi ni miongoni mwa sekta chache zitazofungamana na uchumi wa buluu.

Alisema hivi sasa serikali imeamua kujikita katika maeneo hayo ili kuhakikisha rasilmali zinazopatikana katika bahari zinachangia maendeleo ya uchumi wa wa taifa.

Alisema sekta hizo hapa nchini zitasaidia kupatikana kwa fursa nyingi sambamba na kuinua uchumi wa nchi pamoja na kuinua hali za maisha za wananchi wa Zanzibar.

Sambamba na hayo alisema ajira mbali mbali zitapatikana kupitia sekta hizo na kuongeza kipato kwa wananchi.

Waziri huyo alisema, zipo changamoto mbali mbali ambazo kama zitafanyiwa kazi uchumi wa buluu utakuwa na tija hapa Zanzibar.

Miongoni mwa changamoto hizo ni pamoja na kuwa na sera zilizopitwa na wakati, ukosefu wa mpango wa matumizi ya bahari.

“Hatuwezi kuwa na uchumi wa buluu tukaitumia bahari kama shamba la bibi ni lazima tuwe na mpango madhubuti utaoonyesha namna gani tutaitumia bahari yetu, mpango huu ndio wa mwanzo kabla hujafanya chochote”, alisema.

Aliwaomba washiriki kutoa azimio maalum ambalo litaisaidia serikali ili kufikia mpango wa namna gani wazanzibar wataitumia bahari yao.

Pamoja na hayo alisema ukosefu wa taasisi itayosimamia suala la uchumi wa buluu, ambapo alisema ili kufikia malengo yaliyowekwa lazima kuijenga vyema wizara iliyoundwa na kuweka mikakati ya juu ya namna gani rasilimali zilizopo baharini zitatumiwa ipasavyo.

Akiwasilisha mada juu ya uchumi wa buluu, Saleh Saad Mohammed kutoka Tume ya Mipango, alisema kupitia uchumi wa buluu zipo fursa mbali mbali zinapatikana.

Alisema miongoni mwa fursa hizo ni pamoja na kujengwa kwa bandari ya uvuvi baina ya serikali na sekta binafsi.

Pia alisema lazima kujenga sehemu ya kuhifadhia samaki pamoja na kujenga kiwanja cha utengenezaji wa barafu kwa ajili ya kuhifadhia samaki.

Sambamba na hayo alisema kujengwa kwa skuli za uvuvi zitasaidia wananchi wengi kunufaika kwa kujiajiri wenyewe.

Kwa upande wa Mkurugenzi kutoka Mamlaka ya uvuvi wa bahari kuu Dk. Islam Seif Omar alisema wakati umefika sasa watanzania kuvua katika bahari ya kina kirefu.

Alisema Zanzibar ina rasilimali kubwa ya wavuvi wadogo wadogo lakini alifahamisha kuwa wakiwezeshwa pamoja na kujengewa nyenzo wataweza kuvua katika bahari kuu.