Ni kwa tuhuma za ufisadi, ubadhirifu

NA ABOUD MAHMOUD

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Idara Maalum za SMZ, Masoud Mohammed Ali amewasimamisha kazi baadhi ya maofisa waandamizi katika vikosi vya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Akizungumza na waandishi wa habari huko ofisini kwake Vuga, waziri huyo alisema msingi wa kuwasimamisha kazi maofisa hao unatokana na ripoti ya Mamlaka ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu Uchumi Zanzibar (ZAECA), kuonesha kuwepo kwa ubadhirifu mkubwa wa fedha za umma pamoja na kutowajibika.

Massoud alisema kwa mamlaka aliyokasimiwa na dhamana ya kisheria amemsimamisha kazi Naibu Kamishna wa Kikosi cha Zimamoto na Uokozi Zanzibar, Gora Haji Gora juu ya kadhia mbali mbali zinazomkabili.

Masoud alisema kadhia hizo zinajumuisha taarifa za uchunguzi kutoka Mamlaka ya Kuzuia Rushwa na Kuhujumu Uchumi Zanzibar (ZAECA) ikiwemo ripoti ya awali ya usimamizi wa ujenzi wa jengo la kituo cha Zimamoto huko Kijichame Pemba.

Aidha Waziri huyo pia amemsimamisha kazi Mkuu wa Utawala wa Jeshi la Kujenga Uchumi (JKU) na kupisha uchunguzi juu ya kadhia ya zoezi lenye ukakasi la upigaji wa picha kwa askari na watumishi wa jeshi hilo.

Alisema kadhia nyengine inatokana na ripoti ya awali ya ujenzi wa mradi wa mahanga ya vijana wa JKU iliyotolewa na ZAECA ambapo katika uchunguzi huo umeonesha upotevu wa fedha na ukiukwaji wa sheria na taratibu za manunuzi katika miradi ya maendeleo.

Aidha waziri Masoud amemuagiza mkuu wa KMKM kuwasimamisha kazi na kupisha uchunguzi zaidi mkuu wa bohari kuu ya Makao Makuu ya Kibweni, msaidizi mkuu wa bohari pamoja na msaidizi II wa bohari hiyo.

Wakati huo huo, ameagiza atakaekaimu nafasi ya Mkuu wa Utawala wa fedha kikosi cha Zimamoto na Uokozi kumsimamisha kazi mkuu wa utumishi wa kikosi hicho  kupisha uchunguzi zaidi juu ya kadhia ya zoezi la ukakasi la upigaji wa picha askari na watumishi raia katika kikosi cha zimamoto kwa tumuma za makato ya fedha za askari kwa sababu zisizo na msingi.

Masoud alimuagiza atakaekaimu nafasi ya Mkuu wa Utawala wa Fedha wa kikosi cha Zimamoto na Uokozi kumsimamisha kazi mhasibu mkuu na kupisha uchunguzi kwa kadhia zinazofanana na Naibu Kamishna.

Aidha alimuagiza Kamishna wa Chuo cha Mafunzo kumsimamisha kazi na kupisha uchunguzi zaidi mhasibu mkuu wa chuo hicho kwa tuhuma za ubadhirifu wa fedha zilizowasilishwa na ripoti ya uchunguzi ya ZAECA.

Alisema ubadhirifu huo unatokana na mradi wa ujenzi wa Chuo cha kurekebisha wanafunzi watoto Hanyegwa Mchana Unguja.