NA MWAJUMA JUMA

SERIKALI imesema haitosita kuwachukuliwa hatua waajiri wanaoendelea kuwapa likizo bila ya malipo wafanyakazi wao kwa kisingizio cha maradhi ya corona.

Agizo hilo limetolewa na waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Uchumi na Uwekezaji, Mudrik Ramadhan Soraga huko ofisini kwake Mwanakwerekwe alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari, kuhusu muundo wa suala zima la ajira hasa katika kipindi hichi cha ajira.

Alisema serikali ilitoa toleo namba moja la 2021 la kuwaagiza waajiri kusitisha likizo hizo, sambamba na kuwarejesha kazini ndani ya mwezi huu wafanyakazi wao, lakini bado wapo waajiri wanaendelea kuwapa wafanyakazi wao likizo bila ya malipo na wengine kuwapa mishahara pungufu mpaka kipindi hichi ambacho biashara imeimarika vyema.

Hivyo aliwatahadharisha waajiri wa aina hiyo kuwa serikali haitasita kuwachukulia hatua za kisheria wale ambao wote wataenda kinyume na sheria za nchi na maelekezo ya serikali.

“Ni imani yangu kwamba waajiri wote wataitikia wito na kutekeleza ipasavyo maelekezo ya serikali ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono jitihada za serikali ya awamu ya nane inayoongozwa na Dk. Hussein Ali Mwinyi katika kukuza na kuzilinda ajira za staha zilizopo”, alisema.

Alieleza kuwa mnamo mwezi Machi, Shirika la Afya Duniani lilitangaza uwepo wa maradhi ya corona hatua ambayo ilisababisha nchi nyingi ikiwemo Zanzibar kuchukuwa hatua za tahadhari ikiwemo kudhibiti uingiaji wa wageni.

Hata hivyo, alisema kwa kutokana na hali ya biashara ya utalii kuimarika wizara yake haioni uhalali wa waajiri kuendelea kutoa likizo bila ya malipo ambazo zilitolewa kwa sababu ya janga la corona kwa wafanyakazi wao baada ya mwezi wa Disemba.

Hivyo alisema ni mategemeo ya Serikali kuwa wafanyakazi wote watarudi kazini na kuanza kazi ndani ya mwezi huu wa Januari 2021.

Aidha iliwataka waajiri wote kufanya mazingatio ya kuongeza muda wa mikataba ya kazi ya wafanyakazi wao ambayo iliathirika kwa likizo bila ya malipo za muda mrefu.

Sambamba na hayo waziri Soraga aliwataka waajiri hao kuwalipa wafanyakazi wao viwango kamili vya mishahara kwa mujibu wa toleo la mishahara la mwaka 2017 na kuwashahuri waajiri kufanya majadiliano na wafanyakazi wao juu ya hali ya biashara ilivyo na changamoto zake.

Alisema kuwa kwa sasa Zanzibar imekuwa kituo kikubwa cha utalii na watalii wamekuwa wakiongezeka na kwa mwezi wa Novemba na Disemba 2020 idadi ya watalii waliotembelea Zanzibar ni 77,722 katika kipindi hicho.