NA HABIBA ZARALI

WAZIRI wa Uvuvi na Uchumi wa Buluu, Abdallah Hussein Kombo amesema, serikali ya awamu ya nane ina lengo la kuwasaidia wavuvi kujiendeleza kiuchumi.

Aliyasema hayo katika hafla ya kukabidhi boti za doria kwa baadhi ya kamati shirikishi za usimamizi wa pamoja wa uvuvi jimbo la Mkoani.
Aliwataka wakaazi wa jimbo la Mkoani kudhibiti uvuvi haramu na kumchukulia hatua yeyote atakaepatikana akifanya uvuvi haramu.

“La muhimu ni kuzingatia umuhimu wa boti hizi kwa kuzitunza ili zidumu na kufaidisha wananchi na sio vyenginevyo,”alisema.
Ofisa Mdhamini wizara hiyo, Sihaba Juma Vuai,
aliishukuru taasisi ya MCC kwa kuwapatia boti wavuvi hao ili kulinda rasilimali ya bahari.
Aidha aliwataka kuwa waadilifu kwani azma ya serikali ni kuwasaidia wananchi.

Alisema taasisi ya MCC imeanzisha maeneo ya majaribio kwa kuanzisha mfuko wa kutunza bahari unaojumuisha makundi yote ya uvuvi.
Mkurugenzi wa kampuni ya MCC, Ali Khamis Thani, alisema idara ya uvuvi Zanzibar inafanya kazi na wadau tofauti ikiwemo washirika wa maendeleo  taasisi binafsi kama MCC, mradi wa Swiofish, jamii, serikali za shehia na kamati za uvuvi.
Alisema wanawajengea uwezo wanakamati za uvuvi katika uendeshaji wa kamati na usimamizi wa rasilimali za uvuvi ikiwemo mafunzo ya uongozi na utawala bora.

Nao wavuvi hao walishukuru kwa kukabidhiwa boti hizo na kuitaka wizara ya uvuvi kuwapatia mafunzo. Jumla ya shehia nne zimekabidhiwa boti ikiwemo shehia ya Shidi, Kukuu, Makoongwe na Stahabu.