NA HAFSA GOLO
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Idara Maalum za SMZ, Masoud Ali Mohammed amesema utekelezaji wa agizo la serikali la kutolewa vitambulisho vya ukaazi kwa wananchi lazima lizingatie sheria na taratibu zilizopo.
Alieleza hayo jana katika kikao cha majumuisho ya ziara ya Baraza la
Wawakilishi ya Kamati ya kusimamia ofisi za Viongozi Wakuu
kilichofanyika katika ukumbi wa Kikosi cha Valantia (KVZ) Mtoni, wilaya ya
Magharibi ‘A’. Unguja.
Alisema agizo hilo halipingi wala kubeza sheria zilizopo, hivyo amesisitiza
lazima watendaji wasimamie sheria badala ya kufuata mitazamo mengine.
“Agizo la serikali lisiwe chaka la utoaji wa vitambulisho vya Mzanzibari Mkaazi
kiholela na hatimae kusababisha kuibua changamoto sizizo na tija katika masuala
ya kubeza sheria zilizopo nchini,” alisema.
Hivyo Masoud alizitaka taasisi zinazohusika na usimamizi wa suala hilo pamoja na ofisi za Wakuu
wa Wilaya na Mikoa kuhakikisha watu wanaopatiwa vitambulisho ni watu
wanaostahiki na wenye sifa kwa mujibu wa sheria.
Mbali na hilo katika majumuisho hayo Waziri huyo, alipongeza juhudi zinazochukuliwa na kamati hiyo katika kuibua mambo ya muhimu ambayo yatasaidia kuleta ufanisi wa kiutendaji sambamba na mabadiliko ya maendeleo katika taasisi za serikali.
Aliahidi kufanyia kazi ushauri aliopewa na kamati hiyo hasa ikizingatiwa umedhamiria kusimamia kasi ya maendeleo ya serikali ya awamu ya nane katika kuleta huduma bora za wananchi.
Waziri huyo alisema hatua hiyo itasaidia kuleta ufanisi wa kiutendaji na chachu katika kuleta mabadiliko chanya ya maendeleo na kuimarika kwa uchumi.
Katika hatua nyengine waziri huyo, alisema amekusudia kukaa pamoja na watendaji wake ili kuona njia sahihi ya uwekezaji wa mazingira bora katika soko jipya linalojengwa Kibandamaiti.
Alisema kikao hicho kitatoa uamuzi wa kusitisha ufunguzi wa soko hilo ambao
unatarajiwa kufanyia mapema mwezi wa Febuari hadi mapaka ufanyike ujenzi wa
miundombinu ya maji ya mvua sambamba na vifaa vya kuwekea bidhaa kwa
wafanyabiashara watakaotumia soko hilo ikiwa ni miongoni mwa maombi ya kamati
hiyo.
Mapema
Kaimu Mkurugenzi wa Baraza la Manispaa Mjini, Suleiman Mohamed Rashid, alisema
ujenzi wa soko utakapokamilika zaidi ya wafanyabiashra wadogo 1,200 wanaofanya
biashara zao eneo la Kijangwani na wengine wanaofanya maeneo yasio rasmi
wanatarajiwa kufanya shughuli zao katika soko.
Alisema ujenzi wa soko hilo awali ulikuwa ni wa mabanda 14 lakini kutoka
a na ukubwa wa eneo na mahitaji ya wafanyabiashra, mabanda mengine 14
yameongezwa na kuwa na idadi ya mabanda 28 ambayo anaamini yatapunguza changamoto
ya ufinyu wa maeneo ya biashara.
Rashid aliongeza kuwa changamoto iliyopo katika soko ni ukosefu wa fedha za kujengea
uzio sambamba na miundombonu ya kudhibiti mazingira wakati wa mvua ikiwemo
vigae.
Nae Mkuu wa Wilaya ya Magharibii ‘B’, Hamida Mussa Khamis alisema kukamilika
kwa soko hilo litamaliza tatizo la kuzagaa kwa wafanyabiashara wadogo katika
maeneo mengine ikiwemo Michenzani.
Mwenyekiti wa Kamati hiyo Hassan
Khamis Hafidh, alimtaka Waziri kuhakikisha
zinatumika mbinu mbadala zitakazosaidia soko hilo la muda kuwa ni la kisasa na
kutoa huduma bila ya kikwazo chochote ikiwa ni pamoja na ujenzi wa miundombinu
ya uingiaji wa maji ya mvua na uzio.
Alisema iwapo soko hilo litafunguliwa bila ya kufanyia mambo hayo litaondoa haiba na mandhari nzuri na kutofikia malengo ya serikali.