NA MWANDISHI WETU

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge, Uratibu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu amewapongeza wakulima wa zao la tangawizi na kukemea kilimo cha Mirungi Wilayani Same Mkoa wa Kilimanjaro.

Ametoa pongezi hizo alipotembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa Kiwanda cha Kuchakata tangawizi cha Mamba Miamba kilichopo katika Kata ya Myamba Wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro.

Waziri alifurahishwa na wakulima hao kuwekeza katika kilimo cha tangawizi na kueleza kuwa, ni wakati muafaka kuachana na kilimo cha mirungi kwani Wilaya hiyo imekuwa ikijihusisha na kilimo hicho kwa muda mrefu.

“Wakulima shikamaneni na hakikisheni kilimo cha tangawizi kinakuna na tija na kuachana kabisa na kile cha mirungi, maeneo yenu yana rutuba ya kutosha kwa kilimo yatumieni kuzalisha kwa wingi tangawizi mjikwamue kiuchumi,”alisema waziri Mhagama

Aliongezea kuwa, katika maeneo yaliyokuwa yakimpa shida kwenye mapambano dhidi ya matumizi ya dawa za kulevya aina ya mirungi ni pamoja na wilaya hiyo.

“Faraja ninayoipata leo ni kuona zao la tangawizi sasa linakwenda kuchukua nafasi ya kilimo cha mirungi na niwaombe Kamati ya Ulinzi na Usalama tujitahidi kuhakikisha tunatokomeza ulimaji wa mirungi kwa gharama yoyote”alisisitiza