NA MWANAJUMA ABDI, DAR ES SALAAM

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais Fedha na Mipango, Jamal Kassim Ali amesema Benki ya Dunia (WB), imeahidi kuendelea kushirikiana na serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika kusaidia miradi kwenye sekta za elimu, uvuvi, umeme na kuendeleza miji.

Hayo aliyasema jana, wakati waziri huyo alipofanya mazungumzo na Mkurugenzi wa Benki ya Dunia (WB) wa Kanda ya Tanzania, Malawi, Zambia na Zimbabwe, Dk. Mara Warwick katika ofisi za Uratibu wa Shughuli za SMZ, Dar es Salaam.

Alisema benki hiyo bajeti yake inaishia Juni ya kila mwaka, hivyo utekelezaji wa miradi hiyo utaanza Julai mwaka huu, ambayo itawasaidia kuwajengea uwezo wazanzibari katika vyuo vikuu na vyuo vya amali ili kupatikana kwa wataalamu katika sekta ya uvuvi wa bahari kuu, gesi na mafuta.

Alieleza dunia hivi sasa ina mabadiliko makubwa ya utandawazi wa sayansi na teknolojia hivyo W.B imeahidi kusaidia katika mafunzo ya kuzalishwa wataalamu katika fani mbali mbali kuanzia vyuo vya amali hadi vyuo vikuu katika kufanikisha uchumi wa buluu na kukuza maendeleo.

Aliongeza kuwa uchumi wa buluu unahitaji kupata wataalamu waliobobea katika uvuvi wa bahari kuu, mafuta na gesi, ambapo kuwepo kwa mafunzo katika vyuo hivyo itawajengea uwezo wa kitaalamu watu wa Zanzibar katika kufanikisha sera ya uchumi wa buluu.

Aidha alisema eneo jengine aliyoomba kutaka kushirikiana na Benki ya Dunia, ambayo ni mdau wa Tanzania ni kuwasaidia Bima ya Afya wananchi wa Zanzibar, ambapo Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi alizungumzia kuimarisha huduma za afya kwa wananchi wote.

Waziri Jamal alisema changamoto ya ugonjwa wa corona imesababisha watalii wengi kutoka nchi za magharibi kutokuja Zanzibar, hivyo kumesababisha kupungua kwa mapato.

Alisema Zanzibar inakwenda katika mabadiliko makubwa ya kimfumo na kiuchumi, hivyo kunahitajika wataalamu wengi wa sekta mbali mbali za kiuchumi, kisheria na wataalamu wa ufundi hivyo aliwaomba wanapotoa ufadhili wa masomo wawapatie nafasi vijana wa Zanzibar.

Naye Mkurugenzi wa Benki ya Dunia Kanda ya Tanzania, Malawi, Zambia na Zimbabwe, Dk. Mara Warwick alisema benki hiyo itaendelea kusaidia Zanzibar katika nyanja za kielimu kwa kuwajenga uwezo katika vyuo vya amali na vyuo vikuu ili kuweza kukuza uchumi wa buluu.

Alisema miradi mengine watayosaidia ni nishati ya umeme, uvuvi, kujenga miji ili kuendana na teknolojia ya habari ya mawasiliano (ICT) ambayo ni muhimu katika kukuza uchumi na maendeleo ya wazanzibari.

Aliwapongeza kwa kufanya vizuri katika miradi mbali mbali inayoendelea pamoja na kuwapongeza mradi wa TASSAF III, kwa kupata mafanikio makubwa katika kupunguza umasikini na kukuza uchumi.

Alieleza W.B imekuwa inafanya kazi kwa mashirikiano makubwa na Tanzania katika nyanja mbali mbali hivyo wataendeleza mashirikiano hayo yaliyodumu kwa muda mrefu katika kukuza kasi ya uchumi na maendeleo kwa ujumla.