LONDON, UINGEREZA

SHIRIKA la Afya Duniani, WHO limesema ni mapema mno kuregeza hatua za kukabiliana na janga la corona barani Ulaya licha ya kupungua kwa maambukizi katika nchi nyingi.

Hans Kluge

Mkurugenzi wa shirika hilo kanda ya Ulaya Hans Kluge, alisema nchi 30 kati ya nchi 53 za Ulaya zilishuhudia kupungua kwa maambukizi kwa kiwango kikubwa mnamo kipindi cha siku 14.

Hata hivyo Kluge alisema viwango vya maambukizi kote Ulaya bado vipo juu mno.

Alieleza kuwa mifumo ya afya bado imelemewa na utoaji huduma umeathirika na kwa hivyo ni mapema mno kuregeza vizuizi.

Wakati huo huo, Waziri wa Mambo ya ndani wa Ujerumani Horst Seehorfer alisema nchi yake inajiandaa kupiga marufuku watu wanaoingia Ujerumani kutokea Uingereza, Ureno, Brazil na Afrika Kusini ili kupunguza usambaaji wa aina mpya ya virusi vya corona vinavyoambukiza kwa kasi ambavyo vimeripotiwa katika nchi hizo.

Seehorfer alisisitiza kuwa Ujerumani itaendelea na mipango yake hata kama Umoja wa Ulaya hautokubaliana na hatua za aina hiyo.