LONDON, UINGEREZA
SHIRIKA la Afya Duniani WHO limekadiria kuwa watu zaidi ya milioni saba hufariki kila mwaka duniani kote kutokana na uchafuzi wa hali ya hewa.
WHO ilieleza katika taarifa kwamba uchafuzi wa hali ya hewa ni moja ya sababu kuu za maradhi na watu kushindwa kwenda makazini katika maeneo mbalimbali duniani.
Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Shirika la Afya Duniani, miji ambayo barabara zake zina msongamano mkubwa wa magari na inatumia kiwango cha juu cha fueli ni vituo vikuu vya maradhi yanayohusiana na uchafuzi wa hali ya hewa.
Mark Newhan,Ofisa wa WHO mjini Barcelona, Uhispania alisema, utafiti huo ulithibitisha kuwa miji mingi bado haijachukua hatua za kutosha kwa ajili ya kuondoa uchafuzi wa hali ya hewa.
Kwa wastani, asilimia 84 ya watu wanaoishi katika miji iliyofanyiwa utafiti wanakabiliwa na hatari ya kuathiriwa na chembembe chafuzi za kiwango cha juu zaidi kilichoshauriwa na Shirika la Afya Duniani.
Aidha asilimia tisa ya miji ina kiwango cha juu mno cha chembechembe hizo.