NA JOSEPH NGILISHO, ARUSHA
MKAZI mmoja wa Kijenge Mwanama jijini Arusha, John Tarimo, amelazwa katika hospitali ya mkoa Arusha ya Mount Meru, baada ya kujikata uume na kujaribu kujiua kwa kujinyonga kutokana na ugomvi unaodaiwa ni wivu wa kimapenzi.
Akizungumzia tukio hilo Kamanda wa Polisi Mkoa was Arusha, Salum Hamduni, amethibitisha kutokea tukio hilo na kueleza kijana huyo anapaatiwa matibabu katika hospitali ya Mkoa Mount Meru chini ya ulinzi wa polisi.
“Kitendo Cha kujaribu kujiua ni kosa kisheria hivyo majeruhi huyo anatibiwa katika hospitali ya Mkoa Mount Meru chini ya uangalizi wa polisi na akipona tutamfikisha mahakani kwa kosa la kutaka kujiua”alisema Hamduni
Mtuhumiwa huyo aliacha ujumbe kuwa anajiua kutokana na ugomvi kati yake na mkewe na ndugu zake, Hata hivyo ujumbe huo haukufafanua sababu ya ugomvi huo.
Baadhi ya majirani walioshuhudia tukio hilo wamesema walimkuta Tarimo akiwa hajitambui huku damu zikiwa zimetapakaa eneo la tukio akiwa amejitundika kwa lengo la kupoteza maisha
Mmoja ya jirani na mtuhumiwa Onesmo Mjema amesema Tarimo walimkuta alikuwa amejifungia ndani ya chumba alichokuwa amepanga akiwa ameukata uume na kubaki sehemu ndogo na amejikata mkono huku akitoka mapovu mdomoni.
“Mke wake alikuwa ametoka amemuacha ndani lakini aliporudi akiwa na mtoto wao mmoja alikuta mlango umefungwa ndipo baada ya kuchungulia dirishani alimwona mumewe akiwa ametapakaa damu na anatoka mapovu,” amesema Mjema.
Jirani mwingine walivunja mlango na kuingia ndani kumtoa nje akiwa hawezi kuzungumza huku damu zikimtoka. “Baada ya hapo tulimwita mwenyekiti wa mtaa ambaye alitupa maelekezo tumpeleke hospitali kuokoa maisha,” amesema.
Hata hivyo, mmoja wa majirani aliyeomba kuhifadhiwa jina lake amesema kwa muda mrefu kulikuwa na ugomvi wa wivu wa mapenzi baina ya Tarimo na mkewe ambaye wamezaa naye mtoto mmoja.