NA HAFSA GOLO

SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar, imesema ina mpango wa kuzifanyia mapitio sera na sheria zilizopo ili ziweze kuendana na mabadiliko ya kimaendeleo ya serikali ya awamu ya nane.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Sera, Uratibu na Baraza la Wawakilishi, Dk. Khalid   Salum Mohamed alitoa kauli hiyo alipokutana na waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Watu wenye ulemavu, Jenista Mhagama ofisini kwake Vuga.

Alisema kufanya hivyo kutajenga uaminifu kwa wananchi juu ya kasi ya maendeleo ya serikali yao ambayo wameipa imani kubwa ya kuleta maendeleo ya haraka.

Dk. Khalid alisema kwamba anaamini sera zitapokidhi mahitaji yaliyopo upo uwezekano wa kutimiza malengo ya serikali yaliyokusudiwa kwa muda mfupi sambamba na watendaji na viongozi kuchapa kazi kwa bidii na uadilifu.

Aidha huyo alisema, katika kuhakikisha kunakuwa na mabadiliko endelevu ya maendeleo nchini na kutimiza malengo ya serikali zote mbili watahakikisha wanadumisha mashirikiano ya kiutendaji sambamba na kuibua mbinu zitakazosaidia kasi ya maendeleo.

Akizungumzia juu ya maadhimisho ya sherehe miaka 57 ya Mapinduzi ya Zanzibar Dk. Khalid, alisema maadhimisho hayo yaliyofanyika juzi katika viwanja vya Mnazimmoja yamepunguza kwa asilimia 80 ya gharama.

Naye waziri Mhagama alisema katika kuhakikisha wizara hizo zinaweza kufikia dhamira ya serikali zote mbili ipo haja ya kufanyakazi kwa karibu sambamba na kubadilishana uzoefu.

Alisema kunahitajika kufanya program maalumu ambayo itawashirikisha viongozi na  wataalamu wa wizara mbili hizo ili kujadili na kuona maeneo muhimu ambayo yanahitajika kufanyiwa mapitio na kuleta ufanisi wa kiutendaji kati ya pande mbili hizo.

Mhagama alisema mbali na hayo ni muhimu kwa wizara hizo kujenga utamaduni wa kufanya mapitio ya  sera  na sheria zenye kusimamia masuala ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ili serikali zote mbili ziweze kuleta maendeleo ya haraka.  

“Dk. Khalid nakuahidi  kwamba wizara yangu  itafanya kila linalowezekana katika kuhakikisha wizara hizo mbili zinashirikiana katika kuona maendeleo ya wananchi Watanzania yanafikiwa sambamba na kuondosha kero za muungano”,alisema.

Mhagama alimpongeza  Dk. Khalid kwa kukabidhiwa majukumu mazito katika serikali ya awamu ya nane  jambo ambalo limeonesha wazi umakini na umahiri wake katika kuchapa kazi.