NA ABUUBAKAR KISANDU
MASHINDANO ya 15 ya kombe la mapinduzi yamehitimishwa  Jumatano Januari 13, 2021 ambapo Yanga imetwaa ubingwa, baada ya kuwafunga Simba kwa mikwaju ya penalti 4-3 baada ya  dakika 90 kumalizika 0-0 mchezo uliochezwa saa 2:15 usiku uwanja wa Amaan.

Mara baada ya kumalizika michunao hiyo kwa mwaka 2021 mwandishi wa Makala hii, anajaribu kuelezea baadhi ya dondoo kuhusu mashindano hayo.

1. Yanga ndiyo timu pekee iliyocheza dakika 360 (michezo minne) na kuruhusu mabao machache (bao moja), ambapo Simba ilicheza dakika hizo (360) na kukubali nyavu zake kuguswa mara mbili

2. Simba wanaongoza kucheza fainali mara nyingi kuliko timu yoyote (mara 8) wakifuatiwa na Mtibwa Sugar (mara 6) ambapo Yanga wamecheza fainali (mara 3).

3. Simba na Yanga wamekutana mara tatu  katika mashindano hayo zikiwemo mara mbili  fainali na mra moja  nusu fainali mwaka 2011, walikutana fainali na Simba wakatwaa ubingwa baada ya kuwafunga Yanga 2-0.
Mwaka 2017 walikutana tena kwenye nusu fainali dakika 90 mchezo ukamalizika kwa suluhu ya 0-0 na Simba ikashinda kwa Penalti 4-2, lakini mwaka 2021 walikutana tena katika fainali na Yanga wakashinda kwa penalti 4-3 baada ya dakika 90 kutoka  0-0.
4. Timu za Zanzibar bado zinaendelea kuwa washindikizaji wa mashindano hayo licha ya kuwa yanachezwa katika ardhi ya kwao, kwani katika mara 15 zilizochezwa ni timu  moja tu  pekee ilitwaa kombe hilo kutoka Zanzibar ambayo ni Miembeni mwaka 2009.
5. Mashindano ya mwaka huu Simba imeshinda mabao mengi (mabao 7) ikiruhusu kufungwa mawili wakati Yanga wakishinda mabao mawili tu na kuruhusu kufungwa moja.
6. Kwa mara ya kwanza katika mashindano hayo Simba imemaliza dakika 90 pasipo kupiga shuti hata moja  lililolenga lango la wapinzani wao  Yanga walipiga mashuti  matano yaliolenga lango la Simba.
7.  Miraji Athuman wa Simba ameibuka kuwa Mfungaji bora akiwa na mabao  manne akiwashinda Meddie Kagere pia wa Simba mwenye mabao mawili na Steven Sey wa Namungo mabao mawili, ambapo Mkenya Francis Kahata wa Simba amechaguliwa kuwa mchezaji bora wa mashindano, Mkenya na mlinda mlango wa Yanga Farouk Shikalo ameibuka kuwa kipa bora, baada lango lake kuruhusu kufungwa bao moja  tu katika michezo mine.
Mkenya Joash Onyango wa Simba alichaguliwa kuwa nyota wa mchezo huo wa fainali, hivyo kuwafanya wachezaji wa kigeni kutoka Kenya  kutwaa zawadi katika mashindano hayo.
9. Simba ambayo imecheza fainali  nane  imeshinda tatu  (mwaka 2008,2011 na 2015 na kupoteza 5 (Mwaka 2014,2017,2019, 2020 na 2021) wakati Yanga wamecheza fainali tatu , mbili wameshinda na  moja wamepoteza (wameshinda 2-1 mbele ya Mtibwa Sugar mwaka 2007 na  2021 wameshinda mbele ya Simba kwa penalti 4-3 baada ya dakika 90 kutoka 0-0 na fainali 1 walifungwa na Simba 2-0 mwaka 2011.
10. Azam FC ndo wanaongoza kubeba mara nyingi (5) walishinda mwaka 2012, 2013, 2017,2018 na 2019 wakiipiku Simba SC ya Dar es Salaam iliyotwaa mara tatu 2008, 2011 na 2015, Mtibwa Sugar mara mbili  mwaka 2010 na 2020 na Yanga SC mara mbili 2007 na 2021