MICHUANO ya Kombe la Mapinduzi kwa mwaka huu ilifikia tamati juzi kwa Yanga kufanikiwa kutwaa ubingwa huku ushindani ukionekana kuwa mkubwa na viwango vya wachezaji navyo kuongezeka.
Karibu timu zote zilionyesha uwezo mkubwa huku wawakilishi wa Zanzibar, Mlandege, Malindi, Chipukizi na Jamhuri zikijitahidi kupambana hadi tone la mwisho.


Tunachukuwa nafasi hii kuipongeza Yanga na timu zote zilizoshiriki michuano hiyo kwa namna zilizovyonesha kiwango na ushindani huku zikicheza soka la kufundishwa.
Kwa upande wa pili, pia tunaipongeza kamati ya uandaaji wa michuano hiyo,japokuwa muda ulikuwa mfupi, lakini, kuna kitu kimeonekana ambacho ni muhimu kwa soka letu, ushindani wa kweli.


Kwa kuliamini hili, tunaamini makocha waliokuwa wakifuatilia michuano hiyo watakuwa na faida kubwa ya kuona vipaji ambavyo vinaweza kuwa msaada katika vikosi vyao kwa ajili ya maendeleo ya soka nchini.
Tunaamini hapo mwakani michuano hiyo itawekewa ratiba nzuri ili iweze kushirikisha na timu nyingi zaidi zikiwemo za nje ya Tanzania ili iendelee kuwa bora na yenye mtazamo wa kimataifa.


Kama tunavyofahamu, michuano ya Kombe la Mapinduzi ni michuano inayoendeshwa kwa murtada wa sherehe zenyewe za Mapinduzi ya Zanzibar ya Mwaka 1964 ambayo yalimkomboa Mzanzibari kutoka utawala wa kikoloni na usultani.


Hivyo itapendeza zaidi ikiwa michuano hiyo itawekewa mkakati zaidi wa usimamizi ili iendelee kutoa haiba iliyokusudiwa, kuzipamba na kusherehekea Mapinduzi Matukufu ya ya Zanzibar ya 1964.


Hilo ni moja, lakini, jambo jengine tunalolishauri hasa kwa timu zetu za Zanzibar kuifanya michuano hiyo kama darasa upande wao kwa kujifunza aina ya ushindani unaohitajika huku ikizingatiwa kuwa timu zetu zimekuwa na matokeo mabaya wakati zinaposhikiriki michuano ya kimataifa.
Ni ukweli usiopingika kuwa michuano imekuwa ikivuta hisia za mashabiki wengi kutokana na aina ya ushindani unaoneshwa na timu zishiriki hasa zile zinazotoka nje ya Zanzibar.


Hivyo kwa kuitumia michuano hiyo, klabu zetu zitakuwa na mengi ya kujifunza katika kupata matokeo mazuri ikizingatiwa miongoni mwa wawakilishi wetu hao wanacheza Ligi Kuu ya Zanzibar ambayo ndiyo inayotoa wawakilishi wa kimataifa.
Tunaamini baada ya kujitathmini huko, watajipanga na kuzifanyia kazi kasoro watakazoziona na kujipanga kiushindani zaidi kwa mashindano yatakayokuwa mbele yao.


Tuna kila sababu ya kuienzi na kuifurahia michuano hiyo ya kila mwaka, tukiamini itakuwa njia bora katika kuziimarisha timu zetu kuelekea ushindani wa kimataifa.
Hongera michuano ya 14 ya Kombe la Mapinduzi.