NA KHAMISUU ABDALLAH

CHAMA cha Mapinduzi CCM Zanzibar, kimeishauri serikali kuanzisha mahakama ya mafisadi kama iliyokuwepo Tanzania bara ili mali zilizochukuliwa na wahujumu hao wa uchumi zirejeshwe ikiwemo fedha.

Kimesema wakati umefika kwa Dk. Mwinyi kuanzisha mahakama hiyo ambayo itatumika dhidi ya watendaji wanaotuhumiwa kwa makosa ya ubadhilifu wa mali za umma na ufisadi.

Katibu wa Kamati maalum ya Nec Idara ya Itikadi na Uenezi CCM Zanzibar, Catherine Peter Nao, alitoa ombi hilo wakati akizungumza na vyombo vya habari, hivi karibuni hafla iliyofanyika ofisi kuu ya CCM Kisiwandui.

Alisema kuanzishwa kwa mahakama hiyo kutaondosha muhali kwa wote waliokuwa wakijinufaisha kwa maslahi yao badala ya kuitumikia jamii.

Aidha alisema chombo hicho kitaweza kusaidia kwa kiasi kikubwa kurudisha mali za wananchi na kuongeza heshima kwa watendaji.

Alisema ufisadi ukiendelea kuachiliwa utaendelea kuiangamiza nchi na kuwa janga, hivyo aliwaomba wananchi vyama vya siasa na makundi mengine kuunga mkono vita dhidi ya ufisadi.

Katibu huyo alisema wapo baadhi ya watendaji hawakutekeleza wajibu wao ipasavyo katika serikali ya awamu iliyopita na kwamba hawakumsaidia rais mstaafu, hivyo wanapaswa kushughulikiwa.

Hivyo, aliwasisitiza mawaziri waliopewa dhamana katika serikali ya awamu ya nane kuonesha utiifu uliotukuka na kutofuata njia hizo ili kutorejea walipotoka.

Akizungumzia utendaji wa Dk. Mwinyi tangu aingie madarakani alisema amekuwa muumini mkubwa wa kuondoa ufisadi, ubadhilifu wa mali za umma na rushwa katika serikali.

“Nitashangaa sana kuona mtu katika mitandao ya kijamii anatoa maneno ya kumkatisha tamaa au kumuona mbaya tuunge mkono jambo hili, ili ufisadi uondoke kama ulivyoondoka Tanzania bara,” alisisitiza.

Hata hivyo, alisema Dk. Hussein Mwinyi anaendana na maneno na vitendo vyake kwa yale anayoyafanya juu ya dhamira ya dhati katika kuwatumikia wananchi na kusisitiza kwa methali ya ‘Ada ya mja hunena muungwana ni vitendo.

Alibainisha kuwa CCM imeridhika na utendaji wa Dk. Hussein Mwinyi juu ya ahadi zake katika kuwatumikia wananchi.

Alisema Rais ameonesha dhamira yake ya kuchukua fomu kwa ajili ya kuwatumikia wananchi na kuona Zanzibar inapata maendeleo ya haraka. 

Alibainisha kuwa tangu Dk. Mwinyi alipochaguliwa na wananchi wa Zanzibar amekuwa akionana na makundi mbalimbali hata katika nyumba za ibada ambazo wananchi wengi wapo katika nyumba hizo na kusisitiza suala la amani.

Alisema ni dhahiri kuwa wananchi wa Zanzibar wamepata Rais mwenye kukubalika na kuona Zanzibar inasoga mbele kimaendeleo kwa haraka zaidi.

Alisema Rais Mwinyi ni tofauti sana na hatokuwa tayari kudanganyika kwani anafatilia mwenyewe kila kitu na sio rahisi kumdanganya na kuona kila mmoja anawajibika kwa nafasi yake.