SANAA,YEMENI

SERIKALI ya Yemen imesema miripuko iliyotokea katika uwanja mmoja wa ndege kusini mwa nchi hiyo mapema wiki hii ilitokana na shambulio la makombora lililotekelezwa na waasi wa Houthi.

Serikali hiyo ilisema watu 25 waliuawa na wengine 110 kujeruhiwa na miripuko hiyo iliyotokea katika uwanja wa ndege wa kimataifa mjini Aden siku iliyotangulia.

Miripuko hiyo ilitokea punde baada ya ndege iliyobeba mawaziri kutua katika uwanja huo kutoka Saudia.

Waziri Mkuu Maeen Abdulmalik Saeed aliuambia mkutano wa baraza la mawaziri kuwa uchunguzi wa awali unaonyesha waasi wa Houthi walitekeleza shambulio hilo lililotumia makombora yaliyoongozwa.

Lakini hakutoa ushahidi kuthibitisha kuhusika kwa waasi hao katika utekelezaji wa miripuko hiyo.Waasi wa Houthi hawajatoa jibu lolote rasmi.

Yemen imekabiliwa na zaidi ya miaka mitano ya vita vya wenyewe kwa wenyewe kati ya serikali inayoungwa mkono na Saudia na waasi wa Houthi wanaoungwa mkono na Iran.