NA MARYAM HASSAN

JUMUIYA Zanzibar Association of Agriculture for Poverty reduction (ZAAPOR) imesema itahakikisha kuwa inabadilisha maisha ya wakulima ili kuondokana na kilimo cha kujikimu kwenda kwenye kilimo cha kisasa.

Wito huo umetolewa na Mkurugenzi wa jumuiya hiyo wakati akizungumza na Zanzibar leo huko ofisini kwake Fuoni.

Alisema kufanya hivyo kutaongeza kasi ya upatikanaji wa kipato na kuleta maendeleo kwa wakulima na kuweza kujitosheleza kwa chakula.

Alisema lengo la jumuiya hiyo ni kupunguza umasikini kwa kuwapatia elimu juu ya mbinu bora za kilimo pamoja na kuwapatia pembejeo na mbolea.

Alisema, wanawake wengi hivi sasa wamejikita katika vikundi vya ujasiriamali hasa kilimo, hivyo alifahamisha kuwa ipo haja kwa kuwapatia nyenzo hizo.

Aidha alisema, endapo wakulima watajikita zaidi katika kilimo cha kisasa kutapunguza kasi ya maradhi ambayo yanatokana na vyakula vinavyozalishwa ambavyo hutumia kemikali.

Sambamba na hayo alisema jumuiya hiyo inalengo la kuwaunganisha wakulima wa Zanzibar ili kuwa na sauti ya pamoja katika kutatua matatizo yanayowakabili na kujiletea maendeleo.

Aidha alifahamisha kuwa watahakikisha kuwa wanawajengea uwezo kwa kuimarisha wakulima wapate kuzalisha kwa wingi mazao mengi yaliyobora kwa lengo la kuvutia soko na kupata fedha zitakazoboresha maisha yao.

Pia alisema wataweka utaratibu wa kubadilishana uzoefu juu ya mbinu za kisasa za uzalishaji bora wa mazao ya kilimo na mifugo kwa wanachama.

Alisema wataimarisha uhusiano kati ya wakulima na wafugaji kwa kufanya ushawishi na utetezi kupitia vikundi na mitandao mbali mbali.

Alisema jumuiya yake kwa kuwa imejikita katika kilimo itafanya tafiti mbali mbali juu ya maradhi na mifugo, ili kupata mbegu bora za mazao.