TOKYO,JAPANI

SHIRIKA la habari la Japani limebaini kwamba watu wasiopungua 122 walioambukizwa virusi vya korona wamefariki wakiwa nyumbani ama maeneo mengine kote nchini Japani baada ya hali zao kubadilika ghafla na kuwa mbaya zaidi.

Mamlaka ya Taifa ya Polisi inasema vifo 56 viliripotiwa mwezi Disemba mwaka jana,50 kati ya marehemu wakifariki wakati wa karantini nyumbani kwao ama kwenye vituo vya watu wenye dalili zisizo kali.

Mamlaka hiyo pia inasema kuwa katika baadhi ya visa, watu waliugua lakini hawakutibiwa kwa wakati na maambukizi yao kuthibitishwa baada ya kufariki.

Rais wa Chama cha Magonjwa ya kuambukiza nchini Japani Tateda Kazuhiro,alisema wagonjwa wanaoonekana kuwa tu na dalili zisizo kali wanaweza wakabadilika ghafla na hali yao kuwa mahututi.

Anatoa wito wa kuwepo kwa mpango kazi wa kuwachunguza watu walioambukizwa virusi hivyo mara kwa mara, na kuwatuma katika taasisi za tiba ili kutibiwa iwapo hali zao zitabadilika ghafla.