GAZETI la Zanzibar Leo linalochapishwa na Shirika la Magazeti ya Serikali limetimiza miaka 19 tangu lilipoasisiwa kwa mara ya kwanza mnamo tarehe kama yale mwaka 2002.

Gazeti hilo kongwe katika shirika hilo linalochapishwa kila siku, linatokana na lililokuwa gazeti la NURU ambalo lilikuwa likichapishwa wiki mara moja, ambapo serikali ya mapinduzi ya Zanzibar ya awamu ya sita, iliona ipo haja ya kubadilishwa jina na lichapishwe kila siku.

Kwa sasa Shirika la Magazeti mbali ya kuchapisha gazeti la Zanzibar Leo la kila siku, pia linamachapisho ya kila wiki likiwemo gazeti la Zapoti ambalo hujikita zaidi na habari za michezo, burudani na utalii.

Shirika la Magazeti pia huchapisha gazeti la wiki la Zanzibar Leo Jumapili, gazeti jengine la kila wiki ni Zanzibar Mail, ambalo huchapichwa kwa lugha ya kiingereza na kwamba limelenga kuwapa taarifa wageni ambao huwafahamu lugha ya kiswahili.

Gazeti jengine linalozalishwa na shirika hilo ni Zanzibar Leo Wanawake ambalo huchapishwa kila mwezi, likilenga kuwapa taariza zaidi zinazohusu mambo ya wanawake.

Mbali na machapisho hayo, Shirika pia huchapisha matoleo maalum kulingana na maelekezo na miongozo ya serikali na kila linapoona kuna haja ya kufanywa hivyo kwa ajili ya kuelezea sera za serikali.

Akizungumza na gazeti hili, Mhariri Mtendaji wa Shirika la Magazeti ya Serikali, Yussuf Khamis Yussuf alisema kwa sasa hali ya shirika iko vyema kwani linamudu kuchapisha magazeti magazeti matano pamoja na kuchapisha habari zake kupitia mitandao ya kijamii.

“Kazi yetu kueleza yale yanayosemwa na serikali kuwafikishia wananchi, lakini pia jukumu letu kuzisemea changamoto za wananchi ili serikali zipatie ufumbuzi”, alisema.

Alisema shirika hilo linajivunia kuwa na timu nzuri ya wahariri pamoja na waandishi wanaochipukia ambao wapo tayari kwa kazi na kuwajibika kwa muda wote.

Mhariri huyo alisema kwa niaba ya Bodi ya Wakurugenzi, Manejimenti, Bodi ya Wahariri na wafanyakazi wote aliwatakiwa mapumziko mema ya siku ya sikukuu ya mapinduzi.