NA KASSIM SALUM, OMPR

MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla, alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imekusudia kuirasimisha Bandari ya Shumba, ili kuondosha changamoto zilizopo.

Hemed ,ameeleza hayo wakati akizungumza na Wawakilishi wa Wananchi wa County ya Kwale kutoka Mombasa Nchini Kenya waliofika Ofisini kwake Vuga kwa ajili ya kujitambulisha.

Alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, itaendeleza ushirikiano wake na Nchi ya Kenya, katika Sekta ya Afya, Kilimo, Utalii pamoja na Uchumi wa Buluu Sekta ambazo zimepewa kipaumbele na Serikali chini ya usimamizi wa Rais wake Dr. Hussein Ali Mwinyi.

Hemed alisema, kwa vile Zanzibar ni Nchi ya Visiwa imeshaamua kujikita zaidi katika kuimarisha Uchumi wa Buluu kupitia Bahari kutokana na sekta hiyo kuwagusa Wananchi waliowengi sambamba na kuzitumia vyema Rasilmali zinazopatikana.

Alieleza kwamba, Serikali ya Zanzibar, Awamu ya Nane imeweka mkazo zaidi katika kuwafikishia huduma muhimu Wananchi wake hasa kuinua hali zao za maisha kitendo kitakachowasaidia kuwaingizia kipato cha kujikimu.

Akizungumzia kuhusu suala la Ulinzi na Usalama, Hemed aliwataka Viongozi hao kuendelea kuwakumbusha Wananchi wao juu ya hatua ya kufuata sheria na taratibu kwa kuzingatia nidhamu za uingiaji na utokaji Nchini.

Akitoa shukrani zake kwa niaba ya msafara huo Kiongozi wa Shughuli za Serikali  Bungeni kupitia County ya Kwale, Mwepupheh Jackson Ndoro, amemueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kuwa County ya Kwale imevutiwa na muundo wa Serikali ya Mapinduzi  na hivi sasa wapo mbioni kurekebisha mfumo na muundo wao, ili uweze kutoa huduma bora kwa Wananchi wake.

Mwepupheh alimthibitishia Makamu, kwamba County yake itaendelea kushirikiana na Serikali ya Zanzibar kupitia Baraza la Wawakilishi katika kuona uhusiano wa pande hizo mbili unazidi kuimarika.

County ya Kwale Mombasa Nchini Jamuhuri ya Kenya imekuwa na ushirikiano na Zanzibar kupitia Baraza la Kutunga Sheria la Wawakilishi Zanzibar takriban kwa miongo Mitatu sasa.