NA MWANDISHI

GAZETI la Zanzibar Leo linalochapishwa na Shirika la Magazeti ya Serikali, limetunukiwa tuzo ya gazeti bora linalotumia lugha ya kiswahili kwa ufasaha Tanzania.

Hafla ya utoaji wa tuzo hiyo ilifanyika jijini Dodoma mapema wiki hii ambapo mgeni rasmi alikuwa Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan.

Akizungumzia tuzo hiyo, Mhariri Mtendaji wa Shirika la Magazeti ya Serikali, Yussuf Khamis Yussuf, alisema hayo ni mafanikio makubwa kwa shirika.

Alisema tuzo hiyo itakuwa chachu kwa waandishi wa habari kuongeza weledi katika utumiaji wa misamiati ya lugha ya Kiswahili wakati wanapotekeleza majukumu yao.

Aliwapongeza wafanyakazi wa shirika hilo kwa kujitolea kuihabarisha jamii na kuahidi kwamba magazeti yanayochapishwa na Shirika hilo yataendeleza ujuzi katika matumizi bora ya lugha.

Tuzo hiyo ni sehemu ya maadhimisho ya siku ya Kiswahili, ambayo yalifungwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdallla.